MAKALA YA EDO KUMWEMBE

Diamond na Ngassa nao watalia?

NA EDO KUMWEMBE

MACHOZI yanawalengalenga. Ni huzuni. Watu mashuhuri katika fani wote wanalalamika. Jellah Mtagwa analalamika, Maalim Gurumo analalamika, Rashida ‘Snake Boy’ Matumla analalamika. Wote machozi yanawatoka.......

Wote wanahisi wanaishi katika umaskini tofauti na umashuhuri wa zama zao. Kila mmoja anahisi dunia imemtupa katika shimo la takataka. Hawawaoni tena wale mashabiki waliokuwa wanawazunguka kwa macho ya husuda wakati ule walipokuwa katika ubora wao.

Jellah, mmoja kati ya walinzi bora kuwahi kucheza katika nyasi za viwanja vyetu analia na umaskini huku maradhi ya kupooza yakimsumbua. Huyu ni Mwanasoka ambaye mwaka 1982 picha yake iliwekwa katika stempu za Shirika la Posta nchini.

Maalim Gurumo ameimba muziki kwa miaka 50. Sasa hivi miguu inamuuma na pesa ya tiba inamsumbua. Gari lake la kwanza maishani amepewa na mwanamuziki wa kizazi kipya, Diamond Platinum ambaye ameanza kuimba muziki katika Utawala wa Rais Jakaya Kiwete.

Katika sura iliyonuna na isiyotaka masikhara ya Rais wa awamu ya tatu, Ben Mkapa, bado Rashid Matumla aliitwa Ikulu kupeleka mkanda wake wa dunia kutokana na makali yake ya wakati huo.

Lakini sasa kila kitu kinakwenda kombo. Kuna kila dalili kwamba Serikali inaingizwa lawamani na mashabiki au wahusika wenyewe kwa kile kinachoonekana kutowajali mastaa wa zamani ambao wanatajwa kuwa walilitumikia na kulipa sifa taifa.

Siwezi kuzuia vilio. Lakini nataka tufunuane ubongo. Kuna sehemu ambayo tumekosea, tunakosea, na tunaendelea kukosea. Watanzania walio katika fani mbalimbali wamekosa ujasiri na uthubutu wa kufuata misingi ya sera ya Kibepari inavyohitaji.

Sera za kibepari (Capitalism) ingawa hazisemi wazi lakini zinamtaka mwanadamu awe mbinafsi katika maisha yake ya kila siku na awe makini katika kujijali mwenyewe kwa umakini mkubwa pamoja na Familia yake.

Ni katika Ujamaa tu ndipo ambapo mtu anaishi kwa ajili ya watu wengi waliomzunguka, pamoja na Serikali yake. Wanamichezo wetu na wasanii wamelala katika dunia ya zamani.

Wamelala katika dunia iliyowaaminisha kwamba wao ni wasanii au wanamichezo wa serikali pamoja na wananchi wake. Matokeo yake, matatizo mengi yanayowatokea katika siku za usoni wanayalaza katika mikono ya Serikali pamoja na Wananchi.

Kwa mfano, Mwanamuziki hapaswi kuimba bure katika shughuli yoyote ya Chama na Serikali kwa ajili ya upendo wake. Muziki ni biashara na ni kazi kama zilivyo nyingine. Kuachana na ubinafsi wa Kipato kwa kujali Sherehe za Mwenge wa Uhuru ni kujiandalia njia za umaskini wa baadae.

Kwa wenzetu, kuichezea timu ya taifa kama Jellah alivyofanya enzi zake kunaambatana na mambo matatu. Kwanza ni Uzalendo kwa taifa. Pili ni kuongeza kipato cha pesa, tatu ni kuongeza wasifu (CV) kwa mawakala na macho ya Mameneja wa mchezo huo.

Hili la tatu ni kubwa kwao. Lakini kama unacheza kwa ajili ya kuifurahisha Serikali au Mashabiki waliojitokeza uwanjani, unafanya kosa kubwa la kiufundi katika dunia ya kibepari.

Jaribu kumtazama Rashid Matumla katika ubora wake. Kiwango alichofikia kilimaanisha kwamba Rashid ilikuwa lazima awe na kundi la Wasomi lililomzunguka kwa ajili ya kuendesha jina lake na kulitanua zaidi katika masoko, Matangazo na dunia ya kibiashara ya ngumi.

Ni kwa namna gani alifanya juhudi kuhakikisha hilo? Ni kwa kiasi gani washauri wake walifanya juhudi za kumpeleka Rashid katika anga za Floyd Mayweather, Manny Pacquiao, David Haye na wengineo?

Je kosa alilolifanya Rashid wakati huo, hatuoni kama ni kosa ambalo leo Francis Cheka analirudia? Na wakati ukifika, tutalazimika kuingia katika mkumbo wa kusikiliza kilio cha Cheka na umaskini wake wa wakati huo?

Watanzania tumelala katika dunia yetu peke yetu. Sera za Ujamaa wakati Fulani huwa zinatugharimu kwa sababu tunaamini kuwa mwanadamu yupo kwa ajili ya kuifanyia kazi na kuiburudisha Jamii inayomzunguka. Hatuamini kwamba mwanadamu inabidi uwe mbinafsi na kuitumia fursa aliyonayo kwa ajili ya maslahi yake binafsi na ya watoto wake hili mradi usiwe Mwizi au tapeli.

Leo Mike Tyson amefilisika. Hakuna anayemlilia zaidi ya kujililia mwenyewe. Sijasikia akimlaumu Barrack Obama na Serikali yake. Sijasikia akiilaumu Serikali ya Marekani.

Leo, Paul Gascoigne Gazza amefilisika na amejikita katika ulevi uliotopea. Sijamsikia Gazza akiilaumu FA wala viongozi wa timu alizopitia. Anajua kwamba wakati anacheza soka aliishi maisha yake na aliyatawala maisha yake kwa namna alivyojisikia.

Unaposikia mchezaji yupo katika maongezi ya kuongeza mkataba wake huku maongezi hayo yakichukua zaidi ya miezi sita ni kwa sababu anatetea maisha yake ya uzeeni. Anajua atastaafu mwenyewe, ataishi mwenyewe, atajifia mwenyewe.

Ni nani atakubali kusikiliza kilio cha Diamond Platinum wakati akiwa amechoka? Ni nani atakubali kusikia kilio cha Mrisho Ngassa na ofa alizopata maishani? Wakati wao ni huu na ndio muda wa kutengeneza pesa na kuwekeza katika miradi ya kudumu. Serikali na mashabiki tutaingiaje katika kilio cha wakati huo?

Serikali ni nini hasa? Ni muundo tu wa kiutawala dhidi ya Wananchi. Lakini wanaotawala ndani ya serikali ni binadamu kama sisi. Nao wanakufa, wanabadilika madarakani, na wenyewe pia wana matatizo yao kibao. Ukiililia serikali unamlilia nani hasa?

Tuanze kubadili mtazamo. Waliokosea walikosea, lakini tusiruhusu waliopo wapotee zaidi. Unaimbaje bure katika sherehe ya Serikali? Kwanini unaruhusu Ringtone za simu zijae nyimbo zako bure? Kwanini ukatae ofa ya mshahara wa dola 5,000 kutoka El Marreikh?

Kwanini usikubali kuwa chini ya uangalizi wa kampuni yoyote makini ambayo una mkataba nao wa kisheria? Na kwanini mpaka leo usiwe na Mwanasheria au mshauri wako wa masuala ya kazi zao katika mwelekeo wa kibiashara.

Share this:

 
Copyright © CHIWILEINC. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates