MAAMBUKIZI YA VVU JIJINI DAR ES SALAAM YAPUNGUA.

MAAMBUKIZI YA VVU JIJINI DAR ES SALAAM YAPUNGUA.
Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
18/6/2014. Dar es salaam.

Licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali za udhibiti wa maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi na Ukimwi, Jiji la Dar es salaam limefanikiwa kupunguza kiwango cha maambukizi kutoka asilimia 9.8 za mwaka 2007/2008 hadi kufikia asilimia 6.9 kutokana na jitihada zilizofanywa na serikali zikiwemo za uundaji wa kamati shirikishi za mkoa kudhibiti maambukizi hayo. 

Hayo yamebainishwa  katika taarifa ya hali ya maambukizi ya VVU na Ukimwi iliyotolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es salaam Bi. Terezia Mmbando kwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) Dkt. Fatma Mrisho alipotembelea maeneo mbalimbali ya jiji hilo kuangalia hatua zilizofikiwa katika kupambana na ugonjwa huo.
Akisoma taarifa hiyo leo jijini Dar es salaam Bi. Mmbando ameeleza kuwa janga la Ukimwi ni tatizo la dunia nzima na limekuwa kikwazo cha maendeleo ya jamii hapa nchini na kuongeza kuwa jitihada za kudhibiti maambukizi ya Ukimwi jijini Dar es salaam zimechukuliwa kupunguza maambukizi ikiwa ni pamoja na uanzishaji rasmi wa kamati za kuratibu na kusimamia shughuli za kudhibiti Ukimwi kuanzia ngazi ya mkoa, halmashauri, ngazi ya kata na mtaa.

Amesema jiji la Dar es salaam linakabiliwa na changamoto ya ongezeko la kubwa la watu ikilinganishwa na mikoa  mingine hali inayochangia mwingiliano wa tamaduni, shughulim mbalimbali, masuala ya kijamii,kimila na kiuchumi na kuongeza kuwa kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi 2012 idadi ya watu imefikia  4,364,54, wanaume wakiwa 2,125,786 na wanawake 2,238,755 sawa na ongezeko la asilimia 5 kwa mwaka.

Hali ya VVU na Ukimwi mkoa wa Dar es salaam. Hali ya maambukizi ya Ukimwi katika jiji la Dar es salaam kwa mujibu wa matokeo ya utafiti uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kuhusu viashiria vya Ukimwi na Malaria mwaka 2011/2012 inaonesha kuwa kiwango cha maambukizi ya VVU kitaifa ni wastani wa asilimia 5.1 ambapo maambukizi kwa wanawake ni asilimia 6.2 na wanaume ni asilimia 3.8.

Sababu za maambukizi. Miongoni mwa sababu zinazochangia kuendelea kuwepo kwa maambukizi mapya ya VVU katika mkoa wa Dar es salaam ni pamoja na kasi ya ukuaji wa jiji na shughuli za kibiashara hali inayosababisha mwingiliano wa watu na mahusiano ya kimapenzi pia baadhi ya wakazi kutobadili tabia licha ya kupatiwa elimu ya kujikinga na maambukizi ya ya ugonjwa huo.

Sababu nyingine ni hali ngumu ya uchumi hususani maeneo yenye mkusanyiko mkubwa wa wakazi wa kipato cha chini,kuongezeka kwa vitendo vya ngono isiyo salama hususani maeneo yenye nyumba nyingi za kulala wageni, kumbi za starehe, madangulo na makundi yaliyo katika mazingira hatarishi ya madereva wa magari ya masafa marefu.

Aidha, ngoma za usiku zinazokesha  hasa maeneo ya pembezoni mwa jiji zinazoambatana na unywaji wa pombe kupita kiasi  na uwepo wa makundi maalum ya watu wanaofanya biashara ya ngono na wale wanaotumia dawa za kulevya hali inayowafanya washindwe kutoa maamuzi sahihi ya kujikinga na VVU ni miongoni mwa sababu zinazochangia maambukizi mapya ya VVU.

Hatua zilizochukuliwa kudhibiti maambukizi. Mkoa kwa kushirikiana na halmashauri za manispaa na wadau mbalimbali pamoja na mambo mengine umeendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya namna ya kujikinga na maambukizi ya VVU,kuhamasisha upimaji wa hiari wa VVU pia kuongeza nguvu katika mapambano ya kuzuia maabukizi kutoka mama kwenda kwa mtoto kupitia kliniki za afya ya uzazi. 

Hatua nyingine ni utoaji wa huduma za tiba na virutubisho kwa wagonjwa, kuwahudumia watoto yatima na wale wanaoishi mazingira hatarishi pia kutoa mafunzo ya ujasiriamali na kuhamasisha uundaji wa vikundi vya ujasiriamali kwa wanaoishi na VVU ili waweze kumudu gharama za maisha na uundaji wa vikundi vya sanaa vya vijana kwa ajili ya kutoa elimu ya VVU na Ukimwi kwa vijana walio katika mazingira hatarishi ya maambukizi katika jiji la Dar es salaam

Share this:

Post a Comment

 
Copyright © CHIWILEINC. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates