Mapenzi yamekuwa magumu. Ni mzigo mzito kuubeba. Yanaendelea kujeruhi
wengi, bado ni mateso kwa wengine. Sasa hivi, asilimia kubwa ya watu
inaamini kwamba kupata mwenzi sahihi wa maisha ni ndoto za alinacha. Ni
kamari, ni bahati nasibu.
Maendeleo yamekuja na mambo leo. Kile kinachoonekana ni Uzungu,
kimeathiri kwa kiasi kikubwa ustaarabu wetu. Mila na desturi zetu
vimepokwa na utandawazi uliotujia. Hii inamaanisha kwamba uhusiano wa
kimapenzi wa sasa, hauendani na sura ya utamaduni wetu.
Vijijini kuna unafuu japo na kwenyewe fujo zimeshaingia na mambo
yameshabadilika. Mijini ndiyo matatizo yenyewe. Ulimwengu wa digitali na
fursa za mitandao zinatutia wazimu. Tunataka kuiga mitindo ya maisha ya
wenzetu, matokeo yake tunageuka watumwa wa mapenzi.
Hayakuletwa mapenzi ili yawaumize watu, yapo kwa ajili ya kutoa
faraja ndani ya jamii. Yalivyo ni kwamba baada ya misukosuko ya
kimaisha, vurugu mechi za kusaka riziki na mihangaiko mingine ya
kimaisha, angalau unaweza kusahau yote unaporejea kwa mwenzi wako.
Hata hivyo, mapenzi hugeuka matatizo pale ambapo kazini umeondoka
pakiwa moto, unarudi nyumbani nako pia unakuta moto. Unakosa sehemu ya
kwenda kujishikiza. Faraja inaota mbawa. Hapa ndipo tafsiri ya mapenzi
inapokosa mashiko. Jitazame, muangalie na mwenzako!
Japo ni ukweli usiopingika kuwa mapenzi siku zote hayapo tambarare
hata kwa wenza waliostaarabika, ila katika kundi la mabrazameni na
masistaduu ni mtihani. Kuna usemi kwamba glasi hugongana kabatini,
nakubaliana nao lakini kwa makundi hayo ni pasua kichwa.
Mabrazameni na masistaduu ni zao la mapenzi ya Kichina, yaani
uhusiano bandia. Inawezekana akiwa kwako akajilegeza kama amefika, kumbe
anao wengine wengi. Hili ni janga zito kwa maisha ya sasa. Uaminifu
haupo, uzinzi na usaliti vimekuwa fasheni ya kutukuzwa.
Wengine siyo masistaduu wala mabrazameni, wapo kawaida au pengine
wana muonekano wa heshima mno. Hata hivyo, ukichimbua hulka zao ndiyo
utachoka. Ni wakali wa kuwapanga foleni, akitoka kwa huyu anakwenda kwa
yule. Mapenzi yametawaliwa na rangi ya Shetani.
Wapo wanaobadili wapenzi kwa sababu za tamaa, lipo kundi linaloamini
miili yao ni mtaji wa kupata fedha, wengine shida za maisha
zikasababisha uamuzi huo wa kujidhalilisha, wapo ambao ni tabia. Bila
kugusa huku na huko hatosheki. Makundi yote hayo yamezingirwa na
Ibilisi.
Mume wa mtu, anapewa sifa ya ‘uchapaji’ wa vidosho. Kwamba anajua
kuwapanga kila kona. Nyumba za kulala wageni, anaingia kama nyumbani
kwake. Yaani wanamjua, ni mteja wao hodari. Akifika, wanampeleka kwenye
chumba anachokipenda.
Wapo wanaopiga simu, yaani namba za nyumba za kulala wageni zimejaa
kwenye simu yake. Akijibiwa kwamba Sinza Kumekucha hakuna vyumba,
anapiga Vatican, nako akikosa anajaribu Mori. Inahitaji sala na dua
kuishi na mtu wa aina hiyo. Kuna mawili, kama hatakupa maradhi, omba
usijue tabia yake, atakuua kwa presha..................
Post a Comment