Home
»Unlabelled
» Fedha, uzuri si kinga ya mapenzi, kuna kitu cha ziada
Fedha, uzuri si kinga ya mapenzi, kuna kitu cha ziada
By
Unknown
•
12:46 PM
•
•
WAKATI akili yangu ikianza kupata ufahamu, nilikuwa natatizika na
kuwaza kitu gani hasa katika mapenzi kinaweza kumfanya mtu atulie ndani
ya penzi lake. Niliamini kuwa na fedha ndiyo dawa ya mtu kumtuliza
mpenzi wake au kwa mwanamke kuwa mzuri na mwenye sifa zote, ndiyo dawa
ya kumfanya mpenzi wako atulie.
Baada ya kukua na kuingia katika dunia ya ufahamu wenye mitihani
mingi ya mapenzi, nimegundua kuna utofauti mkubwa katika vitu
nilivyoviwaza.
Wakati nakua, nilikutana na matukio ambayo niliona
kama ngamia kupita kwenye tundu la sindano, lakini baada ya kupevuka,
nilipata majibu ya maswali yaliyonisumbua kipindi kile cha utoto.
Sikuamini
mke wa tajiri kufanya mapenzi na muuza mchicha, mwanaume mwenye mke
mzuri kutembea na changudoa au msichana wa kazi asiyejua kuvaa wala
kuoga.
Baada ya kuingia katika kazi hii ya kukumbushana mambo ya
mapenzi, nilipata maswali mawili ya watu wawili tofauti lakini yalikuwa
na jibu moja.
Mmoja alilalamika ana mke, anamhudumia kila kitu
ikiwemo familia yake lakini alichomlipa ni kutembea na mtu asiye na
mbele wala nyuma. Mwingine alilalamika kuhusu mpenzi wake kutembea na
mwanamke wa nyumba ya pili ambaye haufikii hata mguu wake kwa uzuri.
Kabla
ya kulizungumzia hilo, nirudi kwao kuwaeleza kukosa uamini hakuangalii
katembea na tajiri au mwanamke anayekushinda uzuri, kutoka nje ya
uhusiano au ndoa ni kosa kwa vile penzi ni la watu walioridhiana au
kuoana wakiwemo waliooa wake zaidi ya mmoja.
Leo nawajibu wote kuwa
fedha au uzuri wa mtu havibebi ndoa au uhusiano. Nimekuwa muumini mzuri
wa kuwaeleza penzi la kweli lipo vipi, mapenzi ni upendo wa dhati kutoka
moyoni, kuwa tayari kujilinda na kujiheshimu bila kujali una fedha au
ni mwanamke mzuri.
Mapenzi ni mbegu inayohitaji udongo wenye rutuba
ya upendo ili mbegu hiyo imee. Siku zote mwenye mapenzi ya kweli
humuangalia mtu, si kitu.
Tajiri na fedha zake asipopendwa huwa
katika mateso na kukonda wakati ana kila kitu. Penzi la kweli
halinunuliwi kwa gharama yoyote.
Tabia ya asili huwa sawa na moto
unaowaka kwenye pamba, ukitoa moshi ujue hakuna kilicho salama. Wapo
watu wasiokuwa na mapenzi ya dhati, utakuta mtu anajifanya anakupenda
ukiwa naye lakini mkiachana hana habari na wewe, hata kama mnakaa nyumba
moja na kulala kitanda kimoja.
Mtu anapoamua kutoka nje ya ndoa wakati ndani ana mke mzuri au mume wa ukweli anayempa kila kitu, kuna mawili:
Mosi:
Huenda mwanamke aliyenaye alimtamani kutokana na sura na umbile lake
na hakumpenda kwa dhati. Matokeo yake baada ya kumchoka, mwanamke
huonekana hafai na hukaa naye kimazoea.
Upande wa mwanamke, naye
huenda amekwenda kwa mwanaume kutokana na kujua ana fedha lakini anakuwa
hana mapenzi naye. Hapo lazima atatafuta penzi la nje ili afurahishe
nafsi yake, kwa hiyo watu hawa kutoka nje sishangai.
Pili:
Tabia ya kutoridhika na mpenzi mmoja, watu wa aina hii huwa
hawajisikii kula kitu cha aina moja kwa muda mrefu, lazima atatafuta mtu
wa kumfanya abadili mboga.
Vitu hivi vyote huwa vinawachanganya
watu, hasa wale wanaoamini kuwa mwanaume anapokuwa na fedha au mwanamke
anapokuwa mzuri, ni kila kitu katika mapenzi.
Mapenzi ni bahati, hasa
kumpata uliyemkusudia, basi muombe Mungu utakayemchagua naye awe kweli
amekukubali, hata ukiwa mbali kila mmoja amlindie mwenzake heshima, kwa
kutanguliza uaminifu mbele.
SIMILAR ARTICLES
Post a Comment