Mwandishi wa nakala hii Salma said akiwa na Bi kidude |
FATMA binti
Baraka, maarufu kwa jina la Bi Kidude, ni miongoni mwa wasanii wanawake
wachache ambao ni magwiji wa muziki wa taarabu nchini, ambaye kwa siku
ya leo ataibeba manowari yetu ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo
huadhimishwa kila mwaka ifikapo Machi 8.
Bibi huyu
mwenye sauti nzito na inayopenya vyema masikioni mara anapoimba, ni
mzaliwa wa Zanzibar lakini asili ya kabila lake ni Mmanyema kutoka Mkoa
wa Kigoma, magharibi mwa nchi.
Licha ya kuwa na umri mkubwa
(113) , sauti ya Bi Kidude bado ni nzuri na yenye kuvuta hisia, hasa kwa
mpenzi wa miondoko ya muziki wa mwambao.
Bi Kidude katika nyimbo zake
nyingi amekuwa akiwavutia wengi kutokana na nyimbo zake kubeba ujumbe wa
mahaba kama alivyoimba kwenye wimbo wake ’Ya Laiti napenda pasi kifani’
na wakati mwingine mafumbo kwa lugha ya Kiswahili yenye lengo la
kufikisha ujumbe kwa watu maalumu kama alivyoimba katika wimbo wake wa
’Muhogo wa Jang’ombe’.
Hadi hapo utaona kwamba mtu
mzima huyu anapaswa kupewa heshima katika siku kama hii, hasa kwa
kuzingatia kwamba ni Siku ya Wanawake Duniani.
Historia na asili ya jina
Kidude Fatma Baraka kwa kauli yake, anasema amezaliwa miaka 113
iliyopita huko Zanzibar ambako baba yake mzazi alilowea akitokea Kigoma
(enzi za utumwa), hivyo kabila lake ni Mmanyema, tena mwenyewe anajiita
ni Mmanyema asilia.
Ingawa hafahamu kijiji halisi
alichozaliwa baba yake, Bi kidude anasema babu yake upande wa mama
alikuwa Mngindo, wenyeji wa Kilwa.
“Mimi asili yangu ni Mmanyema
wa Kigoma, baba yangu na mama yangu alikuwa Mngindo, lakini baba yangu
alilowea Zanzibar, ndiyo nasisi tukazaliwa huko mpaka sasa naishi
Zanzibar, lakini mie Mmanyema,” anasema Bi kidude alipozungumza na
Tanzania Daima hivi karibuni.
Anasema jina la Kidude alipewa
na mjomba wake wakati alipozaliwa kwa sababu alikuwa na umbile dogo.
“Nimezaliwa miezi saba... njiti, nililazwa kitandani, nilikuwa mdogo,
mtu hawezi kujua kama kuna kitu kimelazwa.
“Kuna mjomba wangu akaja
akakaa nilipolazwa mimi, akaambiwa angalia usimkalie mtoto, akasema
mtoto gani, ni kidude tu hiki, basi ndo tangu siku hiyo jina
limenieleleza.
Mkongwe huyu wa taarabu
nchini, ambaye kwa miaka ya hivi karibuni amejizolea umaarufu kupitia
tasnia hiyo, anasema katika maisha yake hajapata kuwa na mtoto, ingawa
ameweka bayana kwamba aliwahi kuolewa mara mbili.
Kwa muonekano ni kikongwe
mwenye nguvu zake, anasema katika umri alionao, amepitia misukosuko ya
aina tofauti za maisha. Kifupi, safari yake kimaisha ni ndefu.
Anafafanua kwamba ndoa yake ya kwanza alifunga na Ramadhani Ibrahimu, na wa pili aliitwa Juma Kombo.
“Nimeolewa vyuo viwili, cha
kwanza nikaachika, nimewahi kumfumania mume wangu (nadhani anamaanisha
huyo wa pili), nikampiga kwa mikia ya taa nikamwacha anachuruzika damu,
nikaenda zangu na mpaka leo sijaolewa na wala sina haja ya kuwa na
mume,” anasema.
“Sijisifu, ila miye mpaka
kesho ukiniudhi wallahi sitafuti mtu... nitawatuma watu wakuite, ukifika
mie nimeandaa fimbo yangu, nikikuchapa nayo, ikimpata mtu anasimama
kama anatafuta pesa,” anasema Bi kidude na kuongeza utani, jambo
linalokulazimu kuendelea kumsikiliza bila kuchoka.
Anaendelea kuwausia hususan
wasichana walio katika umri wa kuolewa kwamba wanaume wa sasa hivi si
wema wengi wanapenda kumkuta mwanamke ana kila kitu. “Hakuna wanaume
sasa hivi, hao walikuwepo zamani, siyo leo... leo mwanaume anakufuata,
umlishe, umfanyie kila kitu, waapiii! Wanaume enzi hizo,” anasisitiza Bi
kidude.
Maisha yake na uimbaji Mkongwe
huyu wa taarabu na muziki wa mwambao nchini anainadi siri yake katika
fani kuwa ni kipaji. Katika hilo Bi Kidude anasema ameanza kuimba akiwa
binti wa miaka 10, alipokuwa akitoroka kwao na kwenda nyumbani kwa
marehemu Mtumwa binti Saadi, maarufu Siti binti Saad.
Kadhalika, anatanabaisha
kwamba mafanikio kwa mwanamuziki bora ni yule anayetumia kichwa na dhati
ya moyo wake kwenye kuimba. Anasema kubana au kuibadili sauti wakati wa
kuimba si sahihi, inamtoa mwimbaji kwenye uhalisia wake.
“Mie naimba kwa kutumia
kichwa, si kifua au kubana pua aaa! Sifanyi kama hao wanaojiita waimba
taarabu wa siku hizi, kwanza siku hizi hakuna taarabu. Mimi nina uwezo
wa kuimba bila kutumia karatasi... kwani bendi ya polisi! (kicheko kwa
wanaomsikiliza).
“Enzi zetu taarabu ulikuwa mtu
ukiisikiliza ufanye kazi kupata maana yake kutaka kulinda matusi na
kila mmoja anaweza kuisikiliza popote. Kwanza watu walikuwa wanaanza
kuimba saa nane za usiku, ikifika saa 11 unafungwa muziki. Mie nashangaa
siku hizi taarabu inaanza saa mbili.
“Taarabu ya zamani mtu ulikuwa
ukitisa kichwa taratibu, wanawake tulikuwa tunavaa kwa heshima, si siku
hizi watu mnakatika mabuno (viuno), wanawake wanakwenda bila heshima,
au kwa vile kuna matako ya Kichina?” anahoji mwanamuziki huyo huku
akitoa pakiti yake ya sigara aina ya Embassy na kuvuta.
Kuhusu sigara na uimbaji, Bi
kidude hakubaliani na dhana kwamba inamaliza sauti, badala yake
anashuhudia kwamba ameanza kuvuta akiwa kijana lakini sauti yake haina
mabadiliko.
“Nimevuta sigara mie
hujazaliwa na mpaka sasa navuta sijapata TB wala ugonjwa wa mapafu, leo
unaniambia mbaya! Mbona sijafa?” anahoji mkongwe huyo na kueleza kwamba
alianza kuvuta sigara aina ya Seven Seven, Mkasi, Simba, Kulindondo,
Gundufleki na sasa Embassy ambapo ana uwezo wa kumaliza pakiti moja kwa
siku tatu.
Mbali ya kuimba, pia Bi kidude
ana uwezo wa kupiga ngoma, ikiwa ni baada ya kujifunza kwenye majahazi
wakati akiwa na umri mdogo alipokuwa akitoroka kwenda madrasa (chuo cha
elimu ya Kiislamu).
“Nilikuwa nakimbia nyumbani,
naaga naenda chuo lakini sifiki, nazuga kwa kubeba juzuu yangu kwapani
lakini siendi huko, bali nakwenda kwenye majahazi kufundishwa kupiga
ngoma na tumba,” anasisitiza.
Oktoba mwaka 2005 alipata Tuzo ya heshima ya msanii mwenye mafanikio makubwa iliyotolewa nchini Uingereza (tuzo ya WOMAX).
Aliyebaini kipaji chake Bi
Kidude, anapasua ukweli kwamba mtu wa kwanza kuthamini kazi zake na
kumtafuta hadi kufika alipo alikuwa Rais mstaafu wa Tanzania wa Awamu ya
Pili, Ali Hassan Mwinyi.
Anasema alipokuwa Rais wa
Zanzibar, aliwaomba watu wamtafute Bi Kidude ili apate kumwimbia nyimbo
za Siti, kwa kuwa hakuna aliyeweza kuziba pengo japo kidogo la Siti
binti Saad.
“Ali Mwinyi alikuwa akitafuta nyimbo za Siti binti Saad. Akatumwa Vuai na Khadija Baramia ambao siku nyingi hatujaonana.
“Walipotokea wakaniambia
natafutwa na Ali Hassan Mwinyi, mie nikashangaa, kwa sababu nyumba zetu
zilikuwa zikitizamana milango, nikaona bora niende... nikapelekwa
Bwawani nikatengenezewa chumba kama kuku.
“Teena! Nikawa namwimbia
Mwinyi kule Bwawani akija anaburudika... huko nikakutana na Mariam
Hamdani (dada wa aliyekuwa Waziri wa Fedha, Zakhia Hamdani Meghji)
alikuwa anakuja kunipiga picha anapeleka Ujerumani miye Bi Kidude
sijui,” anasema.
Aidha, anafahamisha kwamba
alipelekwa kwa mara ya kwanza nchini Ujerumani na Mariam Hamdani,
aliyemtambulisha kwa watu mbalimbali ambapo aliweza kusimama kwenye
majukwaa na kutumbuiza.
Kama hiyo haitoshi, Bi kidude
anaongeza kwa kusema Mariam alimpeleka hadi kwa Malkia Elizabeth II
nchini Uingereza. “Yeye ndiye alinipeleka Ulaya, sikujua Kiingereza,
nikawa na mlinzi, miye nimefika hadi kwa Malkia Mtukufu Lizabet
(Elizabeth)... akawa ananisalimia Shikamoo mama Kidude.
“Nimepewa cheo na Mtukufu
Lizabet. Nilipofika anafunua vitabu naona sura yangu nikawa nashangaa,
alinipa kidani cha dhahabu nikaamua kukiuza kulekule Uingereza, maana
ningekuja nacho huku wangeniua,” anasema.
Katika hilo, Bi kidude anasema
alipofika kwenye kasri la malkia alikutana na askari waliofanana na
sanamu, wamevalia viatu vya chuma huku akieleza kwamba hajawahi kuliona
kochi kama aliloliona huko.
“Wakati natoka kwa Mtukufu
Lizabet nilijikojolea ndani ya gari kwa hofu mambo niliyoyaona makubwa,”
anasema Bi Kidude ambaye ni binamu wa aliyekuwa Rais wa Zanzibar,
Salmin Amour.
Akiwa nje ya Tanzania, mkongwe
huyo anaeleza anavyothaminiwa huku akisisitiza kwamba Mkurugenzi wa
Nyumba ya Vipaji Tanzania (THT), Ruge Mutahaba, pia alimsaidia na
kumfikisha alipo.
“Mimi, Ruge miye sikumjua
huku, kanikuta napiga ngoma kwa Shakira, kanipenda akanichukua kaenda
kunikodia hoteli alipojua naimba ndo akanikaribisha ofisini kwake,
tunaongea ananihoji, kisha ananipa pesa anaondoka, mie nabaki hotelini
tena.
“Siwi na shida miye, nakwenda
ofisini kwa Ruge, simuombi mwenyewe ananigawia pesa, ananiuliza upo au
haupo, namwambia narudi Unguja na yeye akija Unguja lazima afike
nyumbani kwangu, anachukua alichonacho ananigawia, simuombi aah!
Ananitumikia yeye. Hii ni mara ya pili anakuja kunichukua kwa ajili ya
tamasha,” anasisitiza huku akimwomba Mungu ambariki mkurugenzi huyo.
Miongoni mwa nyimbo zinazompa
umaarufu Bi kidude hadi sasa ni Muhogo wa Jang’ombe, Yalaiti, Kijiti,
Arebaba na Machozi, Machozi ya huba na nyinginezo.
Anavyoijua Dar es Salaam Bi
kidude anasema anaifahamu vilivyo Dar es Salaam kwa kuwa amefika hapa
enzi za utawala wa Mwarabu wakati wazawa wakitoa kodi ya kichwa.
“Nchii hii kaitengeneza John
Rupia miye niko hapa, mama Haambiliki alikuwa anafanya vichekesho,
nimemlea miye, mama mzazi wa mwanamuziki Shakira nimemlea miye. Hao kina
Mzee Yusuf nimewalea wazazi wao.
“Nimekuja hapa binti
sijaolewa, nimekuja kwa madhumuni ya kuimba taarabu, nilifikia Bagamoyo,
Rais Jakaya Kikwete, kazaliwa mikononi mwangu mie, nilikuwa naishi kwa
Sheikh Ramia.
“Nimewahi kuishi Ajipshini
(Egyptian) kwa miaka tisa,” anasisitiza gwiji huyo wa miondoko ya
taarabu ambaye hivi karibuni alikonga nafsi ya Rais Kikwete na
Watanzania waliohudhuria uzinduzi wa kampeni ya Mradi wa Malaria
iliyokwenda kwa jina la ’Zinduka.’
Post a Comment