Home » Diamond » MWANAMUZIKI DIAMOND PLATNUMZ BAADA YA KUTANGAZA AJIRA SASA AMTANGAZA DEMU ANAYEMPENDA, CHEKI HAPA
MWANAMUZIKI DIAMOND PLATNUMZ BAADA YA KUTANGAZA AJIRA SASA AMTANGAZA DEMU ANAYEMPENDA, CHEKI HAPA
UKIFIKA katika mtaa anaoishi mwanamuziki Diamond maeneo ya Sinza Mori jijini Dar es Salaam utaanza kuhisi kuwa kuna staa anayeishi maeneo hayo, macho ya wengi huanza kumtazama mtu anayeelekea katika geti la nyumba anayoishi msanii huyo. (HM)
Muda wote geti hilo limefungwa. Ili uweze kuingia ndani itakulazimu ubonyeze kengele itakayoashiria kuwa kuna mgeni nje anahitaji kuingia ndani. Hata hivyo hauwezi kupenya kirahisi ndani hadi uulizwe shida yako na kama hauna miadi na mtu yeyote anayeishi ndani ya nyumba hiyo haitakuwa rahisi kuingia.
Mwanaspoti lilitinga katika nyumba ya msanii huyo
na kushuhudia ukimya wa hali ya juu ilhali kuna watu ndani. Baada ya kufunguliwa geti tuliingia ndani na kupokewa na Diamond aliyekuwa ameketi katika sebule iliyonakshiwa na mapambo makini ukutani huku ikiwa na samani chache lakini za gharama kubwa.
Tulitumia saa mbili mfululizo katika mahojiano na Diamond ambaye alifunguka kwa kila swali aliloulizwa na kujibu kwa ufasaha na ufafanuzi mpana.
Mwanaspoti: Utendaji kazi wako ukoje katika muziki?
Diamond: Nina mipango makini katika kazi zangu. Mambo yote lazima yapitie kwa meneja wangu ndipo yanifikie mimi, mara nyingi mtu hawezi kuzungumza na mimi moja kwa moja lazima apite huko na hiyo ndiyo staili ya Diamond. Nimejipanga kuhakikisha nafanya kazi gani, kwa wakati gani na sikurupuki tu, japo katika utengenezaji wa nyimbo zangu naweza nikapata wazo basi hapo hapo nikatengeneza mistari.
Mwanaspoti: Utendaji kazi wako ukoje kuanzia asubuhi hadi jioni?
Diamond: Saa tano asubuhi, nikishaamka kitu cha kwanza ni kwenda 'gym', mara nyingi ni hapa nyumbani kama unavyoona hapo nje kuna sehemu ya mazoezi na sehemu
nyingine zilizopo ndani, mara nyingi hutumia muda wa saa moja. Ifikapo saa sita na nusu huwa naanza kufanya kazi zangu lakini itategemea na ratiba zangu za siku ambazo ndio mwongozo wangu wa kuimaliza siku. Baada ya hapo napumzika kwa muda fulani na baadaye jioni huendelea na kazi na mara nyingi kazi zangu huwa nazimaliza usiku wa manane.
Mwanaspoti: Unalala saa ngapi? Na unalala kwa muda gani?
Diamond: Muda wangu wa kulala mara nyingi ni saa kumi na moja alfajiri na kama sikuwa na kazi nyingi studio basi nitalala saa nane usiku. Muda wangu wa kulala ni saa sita mpaka nane kwa siku. Ila hata kama nikilala mapema kuamka ni saa tano asubuhi ila itategemea na nini ninakifanya siku inayofuata na kama nina kazi maalumu na ya mapema itanilazimu niamke mapema ili kuzikamilisha.
Mwanaspoti: Shughuli gani zinazokuchelewesha mara kwa mara kulala?
Diamond: Ni kurekodi na wakati mwingine shoo. Kwa wiki ninafanya shoo nyingi, kama ni tatu basi siku zote tatu nitalala alfajiri. Siku nyingine zinazosalia ninalala usiku wa manane kwa kuwa huwa nakuwa studio na sehemu nyingine ambazo hunilazimu kufanya kazi kwa kipindi kirefu usiku.
Mwanaspoti: Kati ya usiku na mchana ni muda upi unaopenda kurekodi?
Diamond: Kazi zangu narekodi usiku na ndiyo muda ninaopendelea zaidi. Mara nyingi napenda kurekodi saa 7 usiku ili niwe na muda na saa nyingine ni kuepuka lawama kurekodi mchana, kwasababu vijana wengi chipukizi wataona napendelewa. Unajua ninapoingia studio napenda kufanya kazi kwa muda mrefu, hata hivyo iliyo bora sifanyi bora liende na siwezi kufanya kazi na prodyuza anayenipeleka tu, ni lazima na mimi nipime kama kazi niliyoifanya inakwenda vile ninavyotaka au kama yeye anavyotaka ilimradi tufanye kazi nzuri na iliyo
bora.
Mwanaspoti: Unatumia muda gani kurekodi singo moja na kwa upande wa video ni siku ngapi?
Diamond: Inategemea, inaweza kuwa siku mbili au miezi sita lakini nyimbo nyingi zinatumia muda mwingi kwasababu wakati mwingine naanza halafu napata shoo hivyo inanibidi nipange muda mwingine wa kurekodi. Kuna nyimbo zangu ambazo nilizifanya kwa muda mrefu sana hizo huwa sizisahau ikiwemo Ukimwona, Mbagala, Nataka Kulewa na nyinginezo. Nakumbuka katika kazi nilizofanya kwa muda mfupi ni My Number One nilioufanya kwa prodyuza Sheddy Clever kwa kipindi kifupi sana pamoja na Mapenzi Basi sambamba na Binadamu hizi ni baadhi ya kazi ambazo hazikunipasua sana kichwa kuzikamilisha.
Mwanaspoti: Una prodyuza wako maalumu au studio yako mwenyewe?
Diamond: Sina prodyuza maalumu kila kazi nitakayotaka kuifanya ninatafuta prodyuza yule ninayemtaka hata kama sijawahi kufanya naye kazi. Ninafanya hivi nikiwa na malengo maalumu kwa kujiweka vizuri mimi kama msanii na hata kuwapa nafasi maprodyuza mbalimbali kutia mkono kwenye kazi ya mikono yangu. Ninaogopa kuwa na prodyuza maalumu kwa kuwa najua atanisumbua ikiwa atajua kwamba namtegemea yeye pekee katika kazi zangu. Studio sina kwa sasa ila nina mikakati ya kuwa na studio kwani nimeshanunua baadhi ya vifaa.
Mwanaspoti: Unadhani ndiyo sababu iliyokufanya ukagombana na Bob Junior au Manecky?
Diamond: Hapana haya mambo yalishapita lakini nilijifunza mengi ndiyo maana niliamua kuja na staili hii. Naogopa kubaki kuwa msanii ninayetegemea prodyuza fulani, bila yeye siwezi kufanya muziki, lakini mimi ni Diamond ninaweza kufanya muziki na prodyuza yeyote naye akaonyesha ufundi wake kupitia kazi yangu.
Mwanaspoti: Shoo gani kubwa kuliko zote uliyowahi kufanya ambayo haijawahi kujirudia?
Diamond: Diamond Forever. Hii ilikuwa kubwa sana ambayo sitakaa nikaisahau, ilihudhuriwa na watu wakubwa na maarufu hapa nchini hata hivyo ilikuwa ya kipekee ambayo haijafanana na yoyote ile. Ya pili ni ile ya Dar Live ambayo nilifanya baada ya kushuka katika helikopta ile pia ilikuwa kubwa. Lakini kwa nje ya nchi ni Mombasa na Comoro huko nilifanya shoo kubwa sana ambazo siwezi kuzisahau.
Mwanaspoti: Ni shoo ipi iliyowahi kukuingizia pesa kubwa kuliko zote?
Diamond: Shoo ile ya Mlimani City ya Diamond Forever, ile iliniingizia pesa kubwa sana na tangu pale ndipo nilipoanza kufurahia matunda ya kazi yangu. Nilifanya shoo pia Burundi, Mombasa na Congo shoo hizi ziliniingizia kiasi kikubwa sana cha pesa siwezi kutaja ni shilingi ngapi lakini ni pesa nyingi ambazo sitakaa nizisahau.
Mwanaspoti: Shoo ipi ilikuwa ya bei chee ambayo huwezi kuisahau
Diamond: Kwa kweli siwezi kusahau nilipofanya shoo yangu ya kwanza kubwa mwaka 2009 kwenye Fiesta iliyofanyika Dar es Salaam, ilikuwa ndiyo shoo yangu ya kwanza na kubwa wakati huo nilikuwa natamba na wimbo Kamwambie, ilinichukua muda mrefu sana kujiandaa mimi pamoja na madansa wangu wanne tulilipwa Sh 50,000 lakini sikukata tamaa kwani ilikuwa ndiyo mwanzo wangu wa kujuana na watu wengi na wadau wakubwa wa muziki hapa nchini ambao nilikutana nao kwenye ile shoo.
Mwanaspoti: Kwa hivi sasa ni shoo gani ambayo unaweza kusema kwamba utafanya kwa bei ya chini na ni shilingi ngapi?
Diamond: Shoo ninayoweza kufanya kwa bei ya chini kabisa ni Sh 10 milioni za Kitanzania na hii labda nione anayeniomba nifanye shoo hiyo hayuko vizuri na pengine ni rafiki yangu na hawezi kuninyonya, si hivyo tu itategemea pia ni kampuni gani na ni watu wa aina gani ambao watanitaka nifanye nao kazi.
Mwanaspoti: Kwa kawaida Diamond ni msanii wa gharama gani kwa shoo moja ndani na nje ya nchi?
Diamond: Kwa kawaida shoo moja ninafanya kuanzia Sh15 milioni mpaka Sh20 milioni kulingana na muda nitakaofanya shoo. Pia zile za nje ninafanya kwa gharama ya Dola 20,000 mpaka 30,000 yaani ni Sh32 milioni mpaka 48 milioni hivi kwa fedha za Tanzania na nikiwa huko nahakikisha ninafanya kazi vile inavyotakiwa. Lakini hali ni tofauti inavyokuja shoo ile ya uwanjani yaani hapa nazungumzia shoo kubwa zinazofanyika nje ya ukumbi, hizi natoza Dola 20,000 ambayo ni sawa na Sh32 milioni 32 kwa fedha ya Kitanzania.
Mwanaspoti: Kuhusu madansa wako unawachukuliaje?
Diamond: Ni kama kaka zangu na ninawapenda sana kwani tumetoka nao mbali na wanajua kuwa tunafanya kazi pamoja kutengeneza maisha hivyo ni kama ndugu zangu na tunasaidiana kwenye kila jambo ukizingatia kuwa kile tunachokipata tunagawana. Kwa kweli najitahidi sana kuwaambia hasa kuhusiana na masuala ya kimaisha, nahusika katika maisha yao ya kila siku na nijuavyo mimi nikikosea tu mmoja akapotea kundi langu litakuwa limeharibikiwa maana kila mtu namtegemea kwa upande wake. Kwa sasa wamejenga nyumba zao na wanaendelea vizuri kimaisha hilo ndilo sharti langu lazima wafanye mambo ya maendeleo kwa kile tunachokipata.
Mwanaspoti: Umesafiri nao nchi ngapi, na kwanini unapenda kuambatana nao?
Diamond: Nimesafiri nao sehemu mbalimbali kama Burundi, Comorro na sehemu nyinginezo ambako nimekwenda kufanya shoo, sina tabia ya kusafiri peke yangu hata nikienda Ulaya na hata Marekani lazima niwe nao. Ninapenda kuwa nao kwani ni sehemu ya muziki wangu na imefika wakati nimekuwa nataka mapromota kuhakikisha wanatulipia mimi na madansa wangu kwa ajili ya shoo hasa tutakapojua kuwa shoo fulani itaingiza watu wengi au udhamini mkubwa.
Mwanaspoti: Kuna safari ambayo umewahi kusafiri peke yako?
Diamond: Ziko nyingi, nilienda mwenyewe kutokana na ukubwa wa shoo, lakini ni miaka kadhaa nyuma, baadaye nilijiwekea mikakati kwamba siwezi kusafiri mwenyewe wakati shoo nahitaji kufanya na madansa wangu, awali mapromota walikuwa wagumu kunielewa na wapo waliokataa. Niliachana nao na kuwataka wakishajipanga na kuhakikisha kwamba wanaweza kunichukua mimi na madansa wangu watafanya hivyo.
Mwanaspoti: Umewahi kuwatema madansa?
Diamond: Sijawahi kubadilisha madansa kwa sababu wanajua kazi yao. Ingawa nilikuwa na madansa sita nilipokuwa naanza muziki lakini niliachana na wawili kutokana na utendaji wao wa kazi. Wawili hawa hawakuwa wabunifu kila siku walikuwa na staili ileile, niliamua kuchagua vichwa ambavyo vikikaa na mimi mwishowe tunatoka na kitu makini na chenye kueleweka. Kulikuwa na tatizo pia la kukosea stepu wakati wa shoo hili lilikuwa likinishushia sana hadhi yangu jukwaani, hapo ndipo nilipoamua kuwaondoa.
Mwanaspoti: Kwa upande wa malipo unawalipaje?
Diamond: Ninawalipa vizuri lakini siwezi kutaja kiwango ila ingekuwa kwangu ningetaja, hiyo ni haki yao wao wenyewe kutamka ila mimi siwezi kutaja. Malipo ninayowalipa yapo machoni mwa watu wanaowazunguka, dansa kujenga nyumba kumiliki baadhi ya biashara si jambo dogo, hivyo ninawalipa vizuri. Na hata gharama za kusafiri ndani na nje ya nchi vyote ni juu yangu, malipo tunayoyapata tunagawana.
Mwanaspoti: Unakumbana na changamoto zipi katika kazi yako?
Diamond: Nakumbana na mengi, kwanza unapokuwa msanii unayeongoza lazima upate vikwazo vingi. Nakumbana na watu wengi wanaonichukia na kunitusi bila sababu za msingi, hata hivyo nasingiziwa vitu vingi ambavyo havipo nadhani hii ni changamoto iliyotokana na kufanya vizuri katika muziki.
Wapo ambao wanamwona Diamond anafanya vizuri kwenye muziki badala ya kukaa na kuangalia nimepita wapi na wapi anaanza kutoa lawama kwamba ameibiwa na mengine ambayo kimsingi hayana maana.
Mwanaspoti: Siku za hivi karibuni kuna maprodyuza na wasanii wasiofahamika ambao walijaribu kutengeneza kazi yako ya My Number One na kukutusi kupitia wimbo huo na wapo waliotunga mashairi mengine yaliyozungumzia maisha yako kabla hujawa staa, ulijisikiaje? Na unachukua hatua gani?
Diamond: Awali niliumia sana nilipoibiwa mashairi ya wimbo wangu wa Mbagala, iliniuma sana kwa muda wa wiki nzima uchungu nilioupata siwezi kuuelezea. Lakini baadaye nilikomaa, huwezi amini niliposikia zile nyimbo nilicheka sana kisha nikawadharau sana watu waliofanya hivyo maana nipo kwenye hii tasnia siwezi kuchukia watu wasiojua walitendalo kwani na wao wapo katika kujitafutia riziki. Lakini hata hivyo sheria ya muziki bado haijawa makini hapa nchini
nitachukua hatua gani mwisho wa siku nitaacha kufanya mambo yangu ya msingi na kushughulikia wezi wa kazi zangu ambao hata hivyo hawatabanwa kwa lile walilolifanya.
Mwanaspoti: Msanii yupi hapa Tanzania anakutisha kama hayupo vipi huko nje ya nchi?
Diamond: Kwa hapa Tanzania sijaona mwanamuziki anayenitisha, ila siwezi kujua mashabiki wao ndio majaji, nafikiri kila mtu anaweza kuwa na mtazamo wake. Kati ya wanamuziki ninaowahusudu mimi kwa nje ya nchi hasa Afrika ni P Square pekee, hawa wapo katika nafasi kubwa sana kwenye ubongo wangu na nafikiria ni lini ninaweza kuwafikia, hiyo ndiyo ndoto yangu daima.
Mwanaspoti: Unapokuwa juu ya jukwaa unakumbana na vishawishi vipi ukiwa kama msanii mkubwa?
Diamond: Ninapata vishawishi vingi sana ninapokuwa jukwaani. Kwa kweli ninashawishiwa na wakinadada, mfano kuna mwanamke mmoja ambaye alikuwa mmoja wa mapromota wa shoo nchini Uingereza alitaka kunibusu mdomoni kwa lazima, kitendo kile kilinifedhehesha sana na nilishindwa nifanyeje kwani nipo ugenini na jukwaani ilikuwa ngumu sana kwangu. Wakati mwingine wanawake wanapanda jukwaani ili wacheze na wewe mwisho wa siku wanaingiza mikono kwenye suruali yaani sipendezwi kabisa na michezo ya namna hii.
Mwanaspoti: Umewahi kuibiwa ukiwa jukwaani?
Diamond: Nimeshaibiwa sana hasa katika hizi shoo ndogo ndogo mara nyingi watu wanapanda jukwaani na kuondoka na kitu chako. Nakumbuka nimeshawahi kuibiwa saa, pete ya dhahabu na kuna mmoja alitoa kali ya mwaka yaani yeye alinivua nguo kwa lazima.
Mwanaspoti: Inakuwaje nje ya muziki, unakumbana na changamoto zipi?
Diamond: Kitu ambacho ni changamoto kubwa sana kwangu ni simu yangu ya mkononi. Kila baada ya miezi sita au mitatu nalazimika kubadili namba yangu ya simu, nasumbuliwa sana na watu ambao hata hivyo hawana la msingi la kuniambia. Ni kweli kwamba mawasiliano ni kitu cha msingi na
ninawapenda mashabiki wangu lakini namba yangu inasambaa kwa kasi ya ajabu kiasi kwamba nashindwa kupokea simu za maana kwa kudhani kwamba na hao nao ni wasumbufu.
Mwanaspoti: Ina maana milio yote ya simu hapo ni watu wanakupigia?
Diamond: Yap, unavyoona inalia kila dakika watu wanapiga hapa. Muda mwingi hii simu ninaweka 'silent' yaani haitoi mlio wowote kwani inaita kila dakika.
Mwanaspoti: Tuzungumzie uhusiano wako. Mpenzi wako wa kwanza unamkumbuka? na je uliwahi kumpa shilingi ngapi?
Diamond: Mpenzi wangu wa kwanza kabisa enzi hizo ninajifunza mambo haya sikumbuki vyema jina ila alikuwa anaishi Tandale na mimi pia nilikuwa naishi huko na mama yangu. Sikumbuki kama nimewahi kumhonga maana enzi hizo mimi nilikuwa napewa tu na mama yangu pesa, sikuwa na hela yoyote ya kumpa na ilikuwa ni kwa kipindi kifupi kama miezi minne hivi, hata hivyo tulikuwa tunaibana tu kwa siri nilikuwa mdogo.
Mwanaspoti: Kwanini mliachana?
Diamond: Kwanza nilikuwa sijajua mapenzi ni nini. Hata hivyo haikuwa rasmi na wala nilikuwa sijawa na akili ya kupenda sana na nilikuwa na fikra kwamba ni mchezo tu hivyo tuliachana mapema kwani hata yeye akili yake ilikuwa haijakomaa.
Mwanaspoti: Mpenzi wako uliyekuwa naye kabla ya kuwa staa nasikia uliachana naye baada ya kutoka kimuziki kwa nini?
Diamond: Nilimpenda sana lakini aliniacha kabla ya kutoka. Mpenzi wangu wa kwanza alikuwa anaitwa Sarah Sadick, sijawahi kumuhonga na ndiye mwanamke niliyewahi kumpenda sana. Wakati huo Naseeb Abdul kabla sijawa Diamond nilikuwa nahaha kuhangaika ni vipi nitatoka kimuziki. Msichana huyu ndiye aliyenipa hasira za kufanya muziki kwa bidii zote baada ya kunitema na kuanza kuhangaika na wengine na aliniita majina mengi yasiyo mazuri, kisa sina fedha. Si kwamba nilimuacha bali yeye ndiye aliyeniacha kama zali baada ya wiki kadhaa nikatoka na wimbo Kamwambie, taratibu nikaanza kuwa staa naye akaanza kurudi ila nilishamuondoa moyoni mwangu.
Mwanaspoti: Kwa nini mliachana? Unadhani hakukufaa tena kwa kuwa ulishakuwa staa?
Diamond: Alinisumbua sana kutokana na ugumu wa maisha niliokua nao kwa kipindi cha nyuma hadi kufikia 2009. Nilimpenda sana huwezi amini nilikuwa silali usingizi kwa ajili yake. Nahisi ilitokana na mimi kukosa kazi ndiyo maana ilifikia hatua alinipotezea. Lakini baada ya kupata na kujulikana alinifuata lakini sikutaka tena hata baada ya kuniomba msamaha.
Mwanaspoti: Umewahi kuwa na wanawake wangapi tangu uwe staa?
Diamond: Sikumbuki kwa kweli wapo wengi mno, si unajua tena wapo walionitaka na kunilazimisha nifanye hivyo, lakini idadi kamili siwezi kukumbuka na kila siku nasumbuliwa na hawa wanawake.
Mwanaspoti: Ni wapenzi wangapi ambao umekuwa nao kipindi kirefu na kuwapenda kama wapenzi wako?
Diamond: Nimewahi kuwa na wapenzi wanne katika kipindi chote cha ustaa wangu na sikupenda kubadili ovyo ila wengi wao hawakuweza kutimiza haja ya moyo wangu.
Mwanaspoti: Unaweza kuwataja majina?
Diamond: Ndiyo ila wawili wanafahamika zaidi. Wa kwanza kabisa alikuwa anaitwa Sarah na wa pili alikuwa anaitwa Hawa yule msichana niliyeimba naye katika wimbo 'Nitarejea', huyu alizidiwa ujanja na Wema Sepetu ambaye naye alikuja kuondoka kwangu na baadaye nikawa na Penieli Mungilwa.
Mwanaspoti: Mwanamke yupi unahisi ulimpenda kuliko wote?
Diamond: Mwanamke wangu wa kwanza Sarah Sadick huyu aliniingia sana moyoni sijajua ni kwanini. Lakini nahisi huenda kwa kuwa awali alinipenda kweli kwa kuwa wakati huo sikuwa na kitu. Hata hivyo nahisi ilitokana na mimi kutokuwa bize na wakati huo sikufikiria lolote zaidi ya yeye ilitokana na kutokuwa na kazi ya kufanya. Siku hizi sina mapenzi ya kivilee, nawaza zaidi pesa na ninaihangaikia na zaidi ni muziki wangu, hili ndilo la kwanza kabisa linalonifanya niwe bize mapenzi baadaye.
Mwanaspoti: Umeshawahi kutongozwa na wanawake?
Diamond: Ndiyo, wengi sana tena kuna mmoja kati ya wanawake niliowahi kuwa nao alinitongoza yeye mwenyewe ndipo nikawa naye na nilikaa naye katika uhusiano kwa kipindi kirefu tu. Wanaweza kumfikiria mwanamke fulani lakini huwezi amini ukweli ninao mimi mwenyewe na katu hawawezi hata kumhisi. Ninatongozwa sana kwenye mitandao ya kijamii, facebook, whatsapp, Instagram na kwingineko na wapo wasichana ambao wanatafuta namba zangu za simu na kuanza kunisumbua.
Mwanaspoti: Unapata usumbufu wowote toka kwa wanawake?
Diamond: Ndiyo, wengi sana tena kuna mmoja kati ya wanawake niliowahi kuwa nao alinitongoza yeye mwenyewe ndipo nikawa naye na nilikaa naye katika uhusiano kwa kipindi kirefu tu. Wanaweza kumfikiria mwanamke fulani lakini huwezi amini ukweli ninao mimi mwenyewe na katu hawawezi hata kumhisi. Ninatongozwa sana kwenye mitandao ya kijamii, facebook, whatsapp, Instagram na kwingineko na wapo wasichana ambao wanatafuta namba zangu za simu na kuanza kunisumbua.
Mwanaspoti: Ni mwanamke wa aina gani unataka awe mkeo?
Diamond: Kwanza ninahitaji aijue kazi yangu na ajue kwamba mimi ni mtu maarufu hivyo akubaliane na changamoto mbalimbali atakazokumbana nazo kwa kipindi atakachokuwa ndani ya ndoa, siyo siku mbili anafungasha virago. Pia ajue kwamba nitamsikiliza mama yangu kwanza kabla ya yeye hilo naliweka wazi, yeye ana nafasi yake katika maisha yangu lakini mama yangu nimempa kipaumbele, tatu awe tayari kuishi na mama yangu. Nne awe na akili na mwenye utambuzi na atakayeniongoza katika kazi zangu, sihitaji. Itaendelea…
Chanzo: mwanaspoti
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
Post a Comment