MAAMBUKIZI
YA VVU JIJINI DAR ES SALAAM YAPUNGUA.
Na. Aron
Msigwa –MAELEZO.
18/6/2014.
Dar es salaam.
Licha ya
kukabiliwa na changamoto mbalimbali za udhibiti wa maambukizi mapya ya Virusi vya
Ukimwi na Ukimwi, Jiji la Dar es salaam limefanikiwa kupunguza kiwango cha
maambukizi kutoka asilimia 9.8 za mwaka 2007/2008 hadi kufikia asilimia
6.9 kutokana na jitihada zilizofanywa na serikali zikiwemo za uundaji wa
kamati shirikishi za mkoa kudhibiti maambukizi hayo.
Hayo
yamebainishwa katika taarifa ya hali ya maambukizi ya VVU na Ukimwi
iliyotolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es salaam Bi. Terezia Mmbando kwa
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) Dkt. Fatma Mrisho
alipotembelea maeneo mbalimbali ya jiji hilo kuangalia hatua zilizofikiwa
katika kupambana na ugonjwa huo.
Akisoma
taarifa hiyo leo jijini Dar es salaam Bi. Mmbando ameeleza kuwa janga la Ukimwi
ni tatizo la dunia nzima na limekuwa kikwazo cha maendeleo ya jamii hapa nchini
na kuongeza kuwa jitihada za kudhibiti maambukizi ya Ukimwi jijini Dar es
salaam zimechukuliwa kupunguza maambukizi ikiwa ni pamoja na uanzishaji rasmi
wa kamati za kuratibu na kusimamia shughuli za kudhibiti Ukimwi kuanzia ngazi
ya mkoa, halmashauri, ngazi ya kata na mtaa.
Amesema
jiji la Dar es salaam linakabiliwa na changamoto ya ongezeko la kubwa la watu
ikilinganishwa na mikoa mingine hali inayochangia mwingiliano wa
tamaduni, shughulim mbalimbali, masuala ya kijamii,kimila na kiuchumi na
kuongeza kuwa kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi 2012 idadi ya watu
imefikia 4,364,54, wanaume wakiwa 2,125,786 na wanawake 2,238,755
sawa na ongezeko la asilimia 5 kwa mwaka.
Hali ya VVU
na Ukimwi mkoa wa Dar es salaam. Hali ya
maambukizi ya Ukimwi katika jiji la Dar es salaam kwa mujibu wa matokeo ya
utafiti uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kuhusu viashiria vya Ukimwi na
Malaria mwaka 2011/2012 inaonesha kuwa kiwango cha maambukizi ya VVU kitaifa ni
wastani wa asilimia 5.1 ambapo maambukizi kwa wanawake ni asilimia 6.2 na wanaume
ni asilimia 3.8.
Sababu za
maambukizi. Miongoni
mwa sababu zinazochangia kuendelea kuwepo kwa maambukizi mapya ya VVU katika
mkoa wa Dar es salaam ni pamoja na kasi ya ukuaji wa jiji na shughuli za
kibiashara hali inayosababisha mwingiliano wa watu na mahusiano ya kimapenzi
pia baadhi ya wakazi kutobadili tabia licha ya kupatiwa elimu ya kujikinga na
maambukizi ya ya ugonjwa huo.
Sababu
nyingine ni hali ngumu ya uchumi hususani maeneo yenye mkusanyiko mkubwa wa
wakazi wa kipato cha chini,kuongezeka kwa vitendo vya ngono isiyo salama
hususani maeneo yenye nyumba nyingi za kulala wageni, kumbi za starehe,
madangulo na makundi yaliyo katika mazingira hatarishi ya madereva wa magari ya
masafa marefu.
Aidha,
ngoma za usiku zinazokesha hasa maeneo ya pembezoni mwa jiji
zinazoambatana na unywaji wa pombe kupita kiasi na uwepo wa makundi
maalum ya watu wanaofanya biashara ya ngono na wale wanaotumia dawa za kulevya
hali inayowafanya washindwe kutoa maamuzi sahihi ya kujikinga na VVU ni miongoni
mwa sababu zinazochangia maambukizi mapya ya VVU.
Hatua
zilizochukuliwa kudhibiti maambukizi. Mkoa kwa
kushirikiana na halmashauri za manispaa na wadau mbalimbali pamoja na mambo
mengine umeendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya namna ya kujikinga na
maambukizi ya VVU,kuhamasisha upimaji wa hiari wa VVU pia kuongeza nguvu katika
mapambano ya kuzuia maabukizi kutoka mama kwenda kwa mtoto kupitia kliniki za
afya ya uzazi.
Post a Comment