RIPOTI MAALUM / YA NELSON MANDELA R.I.P 

  Mpigania haki za weusi na alama kuu ya udhalimu wa mfumo wa Ubaguzi wa Rangi nchini Afrika ya Kusini Mzee Nelson ‘Madiba’ Mandela amefariki dunia baada yakuugua kwa muda mrefu kufuatia maambukizi ya mapafu kushindwa kutengemaa kwa muda sasa. Mzee Mandela ambaye kwa miezi kadhaa sasa amekuwa akisumbuliwa na matatizo ya maambukizi kwenye mapafu yake amefariki dunia nyumbani kwake ambako alipelekewa toka hospitali ya Moyo ya Mediclinic mjini Pretoria, chini Afrika ya Kusini baada ya familia yake kuomba kufanya hivyo. Mzee Mandela alipelekwa hospitali hiyo Jumamosi ya tarehe 8 Juni ikiwa ni baada ya kuanza tena kusumbuliwa na mapafu; miaka ya themanini akiwa kifungoni Mandela alipata ugonjwa wa Kifua Kifuu (TB) kutokana na kazi ngumu ya kupasua mawe kama sehemu ya adhabu ya kifungo chake. Aliondoka hospitali hapo Septemba 1, 2012 baada ya familia kuomba hivyo na kuahidiwa huduma nzuri ya kitabibu nyumbani. Wakati anaondoka hospitali hali yake bado ilikuwa ya utulivu kidogo lakini isiyo na mabadiliko makubwa. Mipango ya mazishi ambayo inatarajiwa kuvuta maelfu ya watu na mamia ya viongozi wa kimataifa inatarajiwa kutangazwa punde.


Mandela akiwa na Walter Sisulu gerezeni Kisiwa cha Robben
Bw. Mandela (95) alikuwa Rais wa kwanza mweusi wa Afrika ya Kusini kufuatia kutokomezwa kwa utawala wa ubaguzi wa rangi uliofanywa na Makaburu kwa karibu miaka 400 ambapo watu weupe walijipa haki ya kuwatawala na kuwabagua watu weusi. Kabla ya kuwa Rais wa Afrika ya Kusini Mzee Mandela alitumikia kifungo cha miaka 27 jela ambako pamoja na kazi ngumu aliendelea kuongoza kundi la wapigania haki wengine kudai usawa, utu, na umoja wa Waafrika ya Kusini. Mandela alikuwa ni mfungwa maarufu zaidi wa kisiasa duniani ambapo harakati za kutaka afunguliwe zilipiganwa na wanaharakati sehemu mbalimbali duniani licha ya upinzani wa Serikali ya Afrika ya Kusini na Baadhi ya Nchi za Kimagharibi ambazo zilimuona Mandela kama Ghaidi na mchochezi.

Maisha yake ya awali
Mzee Mandela alizaliwa Julai 18, 1918 katika kijiji cha Mvezo mji mdogo wa Umtatu Jimbo la Cape. Akiwa ni mmoja wa watoto wa Mzee Gadla Henry Mphakanyiswa Nelson Mandela alikulia kwa mamake – mke wa tatu wa Mzee Gadla – katika kijiji cha Qunu ambako pamoja na shughuli nyingine za nyumbani alikuwa mvulana mchunga ng’ombe.

Baadaye alianza masomo ya shule ya msingi na baadaye Sekondari ambapo aliamini kuwa alikuwa anaandaliwa kwa ajili ya utumishi katika nyumba ya Chifu wa Kabila lake la Xhosa kama mshauri. Hata hivyo baada ya kurudi nyumbani kutoka masomoni mwaka 1940 alikuta kuwa Chifu Jongintaba ameandaa ndoa Nelson Mandela pamoja mtoto wa kiume wa Chifu huyo aitwaye Justice walitoroka nyumbani na kwenda kwenye Jiji la Johannesburg. Alifanya kazi kama mlinzi katika Kampuni ya Madini ya Crown lakini alifukuzwa kazi na msimamizi wa pale baada ya kugunduliwa kuwa alikuwa ametoroka kwao.


Mandela akiwa amevaa mavazi ya kabila lake la Xhosa; alitoka katika familia ya kichifu.

Kuingia Katika Siasa
Alipokuwa akiishi kwa muda na mmoja wa binamu zake Nelson Mandela alitambulishwa kwa mwanaharakati wa chama cha ANC Bw. Walter Sisulu ambaye baadaye walifungwa pamoja – Sisulu akitumikia miaka 25 jela. Walter Sisulu alimtafutia kazi ya ukarani katika kampuni ya Wanasheria ya Witkin, Sidelsky and Edelman. Akiwa hapo alifanya masomo ya elimu kwa njia ya Posta ambapo alikuwa anatafuta shahada yake ya kwanza. Mwaka 1943 alihitimu masomo yake ya sheria na kuanza kazi kama Mwanasheria badala ya kurudi kijijini kutumika kwa Chifu. Akiwa ameanza kazi kama Mwanasheria Mandela aliendelea kuwa chini ya uangalizi wa Walter Sisulu ambaye alikuwa anaendeleza harakati za kudai haki za weusi. Akikutana mara kwa mara na wanaharakati wengine nyumbani kwa Sisulu Mandela alikutana tena na rafiki yake Oliver Tambo. Ilikuwa ni katika mikutano hiyo alikutana na mwanamama Evelyn Mase ambaye walianza uhusiano wa mapenzi na baadaye kufunga ndoa yake ya kwanza Oktoba , 1944. Walijaliwa watoto wawili wa kiume na wa kike; wa kiume Madiba “Thembi” Thembikile alizaliwa Februari 1946 na wa kike Makaziwe alizaliwa mwaka uliofuatia lakini alifariki miezi tisa baadaye baada ya kupata maambukizi ya ugonjwa uti wa mgongo.

Mandela na mtoto wake wa kwanza wa kiume Themi
Baada ya uchaguzi wa 1948 ambapo watu weupe peke yao walishirikia vyama vya Herenigle Nacionale Party na Afrikaner Party viliungana na kuunda chama cha National Party ambacho kilikuwa na sera ya wazi ya ubaguzi na kikapisha na kupanua ukali wa sera ya ubaguzi kupitia sheria mbalimbali za ubaguzi wa rangi. Serikali ya Kikaburu ikaja na mojawapo ya Sheria kali kabisa za kupambana na wanaharakati ambayo inajulikana kama Ukandamizaji wa Ukomunisti ya 1950. Sheria hii ilikuwa inashughulikia karibu mambo yote yanayohusiana na kuipinga serikali na ikiwahusu watu wote. Migongano kati ya ANC na Serikali ya Kikaburu ilianza kupamba moto.
Mwaka 1952 Nelson Mandela alikamatwa na utawala wa Makaburu kwa kile kilichodaiwa kujihusisha na vitendo vya Kikomunisti chini ya ile sheria iliyopitishwa miaka michache nyume. Alihukumiwa miezi tisa jela na “kazi ngumu” lakini utekelezaji wa hukumu hiyo ulisitishwa kwa miaka miwili. Lakini mwezi Disemba mwaka huo huo Mandela alipigwa marufuku kuzungumza na zaidi ya mtu mmoja kwa miezi sita. Akiwa kiongozi wa ANC hii ilimaanisha kuwa asingeweza kufanya mikutano na wanachama wake. Mwaka 1953 Mandela na rafiki yake Oliver Tambo walifungua kampuni yao ya Wanasheria katika Jiji la Johannesburg na kuifanya kuwa kampuni ya kwanza ya Wanasheria Weusi katika Afrika ya Kusini. Walijishughulisha na malalamiko mbalimbali ya wananchi hasa yanayohusiana na ukatili wa kisiasa. Hata hivyo serikali ikitumia sheria nyingine ikalazimisha kufungwa kwa ofisi hiyo iliyokuwa na wateja wengi na kuihamisha sehemu nyingine ambapo ilikuwa ni vigumu kwa wateja kuifikia. Mwaka 1955 Mandela na wenzake walishirikiana kuandaa kongamano kubwa la watu wa Afrika Kusini ambao wanaamini katika taifa moja la watu wamoja japo wanatoka katika makabila na rangi mbalimbali. Katika kongamano hili kulisainiwa kile kinachoaminika kama mojawapo ya nyaraka muhimu kabisa za kutetea usawa na utu wa watu wote ambayo ilijulikana kama Freedom Charter. Kufananisha hii ni sawasawa na Azimio la Uhuru la Marekani au ile nyaraka ya Waingereza ya Magna Carta. Kwa Tanzania tunaweza kufananisha kabisa na Azimio la Arusha. Freedom Charter ilitengeneza ramani ya kujenga taifa la watu walio huru na sawa katika Afrika Kusini.


Nelson Mandela na Oliver Tambo – wanasheria

Marafiki wawili – miaka mingi toka Kisiwa cha Robben
Hata hivyo kwa upande wa familia ndoa yake kwa Evelyn ilianza kuwa matatani. Kulikuwa na tuhuma za kukosa uaminifu ambapo alidaiwa kuwa na mahusiano ya mapenzi na baadhi ya kina dada wa ANC. Evelyn alijaribu watengane lakini pamoja na jitihahada mbalimbali za kupatana Nelson Mandela aliamua kupeana talaka na mke wake wa kwanza mwezi Machi 1958. Walikuwa wamejaliwa mtoto mwingine wa kike. Wakati huo wa mchakato wa talaka Nelson Mandela alikuwa ameanza mahusiano na Winnie Madikizela mmoja wa wafanyakazi wa mambo ya kijamii. Walifunga ndoa Mwezi Juni 1958.


Ndoa ya Madiba na Winnie
Migogoro na utawala wa kikaburu haikukoma. Na Mandela alizidi kuwa na siasa za mrengo wa kushoto. Njia za amani za kupata mabadiliko ya kisiasa zilionekana kutozaa matunda; Mandela na wenzake walianza kuamini katika njia za kimapinduzi na za kutumia silaha. Hili lilimletea matatizo zaidi na watawala wa Kikaburu. Hatimaye Augusti 2, 1962 Nelson Mandela alikamatwa na utawala wa Makaburu na kushtakiwa kwa kuchochea mgomo wa wafanyakazi na kuondoka nchini bila kibali. Mandela alijiwakilishi mwenyewe mbele ya mahakama huku akitumia nafasi hiyo kutoa hutuba motomoto za kisiasa dhidi ya utawala wa kibaguzi wa makaburu. Alikutwa na hatia na kuamuriwa kufungwa miaka mitano jela; wakati anatoka mahakamani mashabiki wake walisimama pembeni na kuimba wimbo wa Mungu Ibariki Afrika (Nkosi Sikeleli Afrika).

Kesi ya Rivonia

Matatizo yake hayakufikia mwisho. Julai 11, 1963 polisi walivamia shamba la Lilliesleaf – mji mdogo wa Rivonia nje ya Johannesburg) ambapo pamoja na vitu mbalimbali waliamini walikuta ushahidi wa kutosha kumhusisha Mandela na mipango ya kuipindua serikali. Mandela na wenzake walitumia shamba hili kama sehemu yao ya kujificha huku Mandela akijifanya ni mtunza bustani. Kesi hii ilikuwa motomoto kwani Mandela na wenzake walishtakiwa kwa makosa manne yakiwa ni ya uhujumu wa miundo mbinu ya nchi (vitendo zaidi ya 200) pamoja na kutaka kupindua serikali; serikali ilikuwa inapendekeza kuwa wakikutwa na hatia basi wahukumiwe kifo. Mashahidi wengi wa serikali waliitwa pamoja na lundo la ushahidi wa picha na nyaraka kuthibitisha mashtaka ya serikali dhidi ya Mandela na
wenzake tisa.


Mara baada ya kuachiliwa mwaka 1990 Mandela alihakikisha anamtembelea rafiki yake mpenzi Oliver Tambo aliyekuwa anapata matibabu Sweden
Wengine ambao walikuwa pamoja na Mandela ni pamoja na Walter Sisulu na Govan Mbeki (baba yake na Thabo Mbeki aliyemrithi Mandela kama Rais wa Afrika ya Kusini). Ilikuwa ni katika kesi hii ambapo Mandela alitoa mojawapo ya hotuba zinazosifiwa zaidi duniani na ambayo inasomwa na wanafunzi wa siasa sehemu mbalimbali duniani kwani ilielezea falsafa ya kupinga ubaguzi wa rangi. Inafanana sana kimaudhui na barua ya Martin Luther King Jr akiwa katika jela ya Birmingham huko Alabama ambapo alielezea kwanini alikuwa anapinga kubaguliwa na kwanini kila mpenda haki duniani anapaswa kufanya hivyo hivyo. Katika hotuba hii inayojulikana kama “I’m Prepared to Die Speech” Mandela alisema kuwa alikuwa anapigania haki ya watu weusi kuheshimiwa kutokana na utu wao na kuwa wao ni sawa kama binadamu wengine.

Alisema kuwa hapiganii haki ya weusi kuwabagua weupe bali haki ya watu wote kuishi kwa pamoja kama watu wa jamii moja. Mandela alisema “This is the struggle of the African people, inspired by their own suffering and experience. It is a struggle for the right to live. I have cherished the ideal of a democratic and free society, in which all persons live together in harmony and with equal opportunity. It is an ideal which I hope to live for and achieve. But, if needs be, my Lord, it is an ideal for which I am prepared to die”. Yaani, “Haya ni mapambano ya watu wa Afrika yaliyotokana na mateso na mang’amuzi yao wenyewe. Haya ni mapambano ya kupigania haki ya kuishi. Nimelifurahia wazo la jamii ya kidemokrasia na huru, ambapo watu wote wanaishi katika amani na haki sawa. Ni wazo ambalo ninatumaini kuishi kwa ajili yake na kulitimiza. Lakini, ikibidi, mheshimiwa, ni wazo ambalo

nimejiandaa kufa kwa ajili yake”

Baada ya kuhukumiwa kifungo cha maisha Mandela na wenzake wakitoka Mahakamani

Pamoja na utetezi wake wote timu ya Mandela ilishindwa kesi hii na wote wakakutwa na hatia isipokuwa mmoja. Kwa vile tayari kulikuwa na mwamko sehemu mbalimbali duniani kupinga adhabu ya kifo Mahakama ikawaamuru Mandela na wenzake kutumikia kifungo cha maisha na huo ndio ukawa mwanzo wa kifungo cha karibu miaka 30 jela (ikumbukwe kesi hii ilipoanza Mandela tayari alikuwa anatumikia ile hukumu ya miaka 5 jela). Mandela na wenzake walipelekwa katika jela ya Kisiwa cha Robben ambako pale peke yake alitumikia miaka 18. Maisha kifungoni Kisiwa cha Robben na kwingine


Kisiwa cha Robben ambako Mandela alifungwa kwa miaka 18
Mandela na wenzake walihukumiwa kazi ngumu vile vile na kweli ilikuwa ni kazi ngumu kwani pamoja na kuponda mawe walipewa baadaye kazi ya kuponda mawe ya chokaa. Kwa muda alikatazwa kuvaa miwani ya jua kitua mbacho kilimsababishia ubovu wa macho ambao hakuweza kupona kabisa. Akiwa kifungoni mamake alimtembelea mwaka 1968 na siku chache baadaye alifariki dunia, mwaka uliofuata mtoto wake wa kwanza Thembi alifariki katika ajali ya gari – Mandela hakuruhiswa kuhudhuria mazishi yao wote hao. Maisha kifungoni yalikuwa magumu kwa kila kipimo licha ya maisha baada ya miaka kuanza kuboreshwa kidogo kufuatia maandamano na harakati za kutaka Mandela afunguliwe. Utawala wa makaburu hawakusikia la mtu yeyote hasa kwa vile walikuwa wanaushirika wa karibu na serikali ya Marekani na Uingereza ambazo zote zilimuona Mandela kama Mkomunisti na Ghaidi.


Mwaka 1966 gerezani Mandela anaonekana akiitia viraka nguo yake ya jela

Mandela alitumikia pia katika magereza ya Pollsmoor huko Cape Town na Gereza kati ya 1982 hadi 1988 na baadaye gereza la Victor Verster 1988-1990 ambako kwa kiasi kikubwa alikuwa amepewa maisha ya unafuu (hapa chini akiwa na mpishi na huduma mbalimbali) kulinganisha na alivyoishi katika gereza la Kisiwa cha Robben.


Akiwa gereza la Victor Verster alipewa nyumba na mtumishi. Hapa pichani na aliyekuwa mpishi wake kwenye gereza hilo.

Ikumbukwe miaka aliyokuwa Robben ndiyo ilikuwa migumu zaidi kwani hakuruhusiwa kutembelewa na watu wengi na alipewa nafasi ya kutembelewa na kuandikwa barua moja tu kila baada ya miezi sita. Katika magereza hayo mengine Mandela alipata unafuu kidogo.

Kuingia kwa F. W. de Clerk na kuachiliwa kwa Mandela
Chini ya utawala wa Pieter Botha Afrika ya Kusini ilizama katika siasa na sera za ubaguzi wa rangi. Botha aliwachukia weusi na aliamini kabisa kuwa utawala wa kikaburu utadumu kwa muda mrefu. Botha anaweza kabisa kufananishwa na aliyekuwa Gavana wa Alabama George Wallace ambaye aliapa kuwa “ubaguzi sasa, ubaguzi kesho, ubaguzi milele”; japo aliishi na kuona Ubaguzi ukifumuliwa katika jimbo lake na katika Marekani sera hizo zikitupwa katika mifumo ya utawala. Hata hivyo alikuwa ni F. W. de Clerk mwanasiasa mwingine mzungu ambaye licha ya kutoka katika chama kilichoamini katika ubaguzi wa rangi yeye mwenyewe alijikuta akiukataa kifikra kwani aliona hauwezi kudumu.

Kwa muda hivi tangu 1988 Mandela alikuwa na mazungumzo ya siri na baadhi ya viongozi wa serikali juu ya masharti ya yeye na wenzake kuachiwa huru na mwelekeo wa siasa za Afrika ya Kusini. Mazungumzo hayo yalikumbana na vikwazo vingi sana ikiwemo kutokukubaliana kwa masharti – kwa mfano serikali ilitaka Mandela asijiingize kwenye siasa na kuwa wasilazimishwe kuwa na utawala wa wengi (majority rule) masharti ambaye Mandela aliyakataa.

Baada ya Mdahalo mzito ambao de Klerk alionekana kushinda; Mandela alipompa mkono alionekana kushangaza umati wa watu na kujenga daraja kati yake na de Klerk kwa maisha.

Matokeo yake ni kuwa Mandela na wenzake waliachiliwa huru na utawala lwa De Clerk Februari 2, 1990 na kuleta furaha wanaharakati pote duniani. Ikumbukwe kwa Tanzania wimbo maarufu wa “Kilicho cha Wapenda Haki Duniani Kote” ulivuma sana wakati huo katika kuhamasisha Mandela na wenzake waachiliwe huru. Baada ya kuachiliwa huru muda mrefu ulitumika kufanya mazungumzo na utawala wa kikaburu kuhusiana na mwelekeo wa siasa za Afrika ya Kusini na hata kuelekea uchaguzi mkuu. Hata hivyo kutokana na matukio mbalimbali ya vurugu na mauaji ya kisiasa yaliyokuwa yanaendelea na hata migongano ya chama cha Inkatha cha Chifu Buthelezi Mandela aliona hana jinsi isipokuwa kufikia makubaliano ya msingi. Baadhi ya makubaliano hayo yalihusisha kufunguliwa kwa wafungwa wa kisiasa, kuitishwa kwa uchaguzi mkuu, kuwa na Katiba ya Mpito na kuhakikishia kuwa kazi za weupe hazitafukuzwa kama ukiingia utawala wa weusi.Mandela na de Klerk walitunukiwa tuzo ya Nishani ya Amani ya Nobel mwaka 1993 Mandela na de Klerk wakionesha nishani ya Nobel

Uchaguzi Mkuu wa 1994

Hatimaye Afrika ya Kusini ikaingia katika uchaguzi mkuu wa kwanza huru na wawananchi wote mwaka 1994, Aprili 27. Kampeni ilikuwa na vurugu za hapa na pale lakini kwa ujumla wananchi wa Afrika ya Kusini hasa weusi walijikuta kwa mara ya kwanza wanapiga kura kumchagua kiongozi wanayemtaka. Mandela akiongoza ANC walishinda asilimia 62 ya kura na kushindwa kupata theluthi mbili ambayo ingewawezesha kuweza kubadili Katiba. Serikali yake ilikuwa ni ya umoja wa kitaifa ikitegemea kwa kiasi kikubwa baadhi ya maofis waliokuwa katika utawala wa kikaburu. De Clerk alikuwa Makamu wa kwanza wa Rais na Thabo Mbeki akiwa Makamu wa Pili wa Rais. Mandela (katikati) akiwa na Makamu wake wawili
Mandela alishaeleza toka awali kuwa atagombea kipindi kimoja tu na ndivyo alivyofanya na baadaye kumwachia Thabo Mbeki kama Rais wa Afrika ya Kusini. Baada ya kustaafu siasa Mandela aliamua kujishughulisha na program mbalimbali za ndani ya Afrika ya Kusini na kutembelea baadhi ya nchi. Hata hivyo udhaifu wa mwili uliotokana na magonjwa na uzee ulimzidia na kumfanya apunguze safari za nje. Kwa mara ya mwisho alionekana katika shughuli za hadhara katika mashindano ya Kombe la Dunia mwaka 2010 ambayo yalifanyika Nchini Afrika ya Kusini.

Mandela na Tanzania

Tanzania kama nchi imehusika kwa kiasi kikubwa sana katika kuuvunja vunja utawala wa kikaburu na katiak kuongoza harakati za kutaka Mandela aachiliwe huru. Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere na utawala wake mara baada ya Uhuru 1961 aliazimia kutoa msaada wote unaohitajika kwa wapigania uhuru wa Afrika ya Kusini. Kama ilivyodokezwa hapo juu kuwa mojawapo ya mashtaka dhidi ya Mandela ni lile la kwenda nje ya Afrika ya Kusini bila kibali. Mwaka 1962 Mandela akitumia njia za panya alitoroka Afrika ya Kusini na hatimaye kuingia Tanganyika na kukutana na Mwalimu Nyerere ambaye aliwapa ahadi ya ushirikiano mkubwa. Mandela mwenyewe akizungumza katika dhifa aliyomwandaliwa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere mwaka 1997 Oktoba 17; alisema “Inanyenyekesha kukumbuka mchango wa Mwalimu Nyerere katika ukombozi wa bara letu na Uhuru wa Afrika ya Kusini”.


Aliendelea na kumsifia Nyerere kwa kusema kuwa wakati watu wengine walikuja baadaye kuona ubaya wa utawala kikaburu Nyerere aliliona hili mwaka 1959 ambapo akishirikiana na Fr. Huddleston walianzisha harakati za kupinga ubaguzi wa rangi (anti-apartheid movement) ambao zilikuja kuwa maarufu sana baadaye – hasa baada ya kesi ya Rivonia. Mandela alisema kukutana na Mwalimu mwaka 1962 kulimuonesha jinsi Nyerere alivyokuwa anataka haki sehemu zote duniani na jinsi alivyojitoa yeye na taifa lake changa kuona kuwa Afrika yote inakuwa huru.

Wanaharakati – wakisherehekea miaka 80 ya Askofu Trevol Huddleston, Nyerere, Askofu Mkuu Desmond Tutu na aliyekuwa Katibu wa Jumuiya ya Madola Shirdath Ramphal

Katika kuonesha hili Mandela alichagua Tanzania miongoni mwa nchi za kwanza kutembelea mara baada ya kuachiliwa huru mwaka 1990. Aliingia nchini Machi 7, 1990 na kupokelewa na maelfu ya watu wakiongozwa na baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere pamoja na Rais Ali Hassan Mwinyi. Wakati anatembelea nchini kama mtu huru Tanzania ilikuwa na wapiganaji karibu 10,000 wa Afrika ya Kusini waliokuwa wanaishi Tanzania na kujihusisha na mambo mbalimbali. Ikumbukwe ANC ilifungua ofisi yake ya kwanza nje ya Afrika ya Kusini Jijini Dar-es-Saalam mwaka 1961 na hii ilichangia baadaye pia kwa ofisi za vyama vingine vya ukombozi kuchagua Dar kama makao yao makuu. Yote haya yalisaidia kuifanya Tanzania kuwa makao makuu ya Kamati ya Ukombozi ya Nchi Zilizo Mstari wa Mbele ambayo kwa muda mrefu iliongozwa na Brig. Hashim Mbita. Uhusiano huu wa karibu wa Tanzania na Wapigania Uhuru ulithibitika zaidi baada ya Tanzania kuwapatia wapigania uhuru hao maeneo ya mafunzo ya kijeshi na taaluma mbalimbali huko Morogoro eneo la Mazimbu na maeneo mengine Mtwara na sehemu nyingine nchini. Pamoja na vyuo wapigania uhuru hao walipewa maeneo ya shule za msingi na sekondari vile vile.


Wakufunzi wa chuo cha ANC Mazimbu Morogoro enzi hizo


Uhusiano huu wa karibu wa Tanzania na wapigania uhuru wa Afrika ya Kusini ulionekana pia wakati wa Mkutano wa Mawaziri Wakuu wa Nchi za Jumuiya za Madola uliofanyika London, Uingereza . Katika makala yake aliyoandika kwenye gazeti la The Observer Machi 7, 1961 Nyerere aliweka msimamo wa Tanganyika mapema kabisa kuhusiana na uanachama wa Afrika ya Kusini kwenye Jumuiya hiyo (Afrika ya Kusini iliomba kuwa mwanachama na mawaziri wakuu walitakiwa kuchukua uamuzi). Katika makala hiyo Nyerere alisema mojawapo ya mistari inayokumbukwa sana kuwa “kuipigia kura Afrika Kusini ijiunge ni kutupigia kura sisi kujitoa (To vote South Africa in, is to vote us out) na inaaminikuwa kuwa hoja aliyoijenga ilichangia sana kubadili upepo na kusababisha Afrika ya Kusini kutoa ombi lake la kujiunga. Uhusiano wa karibu wa Nyerere na Mandela haukushia wakati huo tu; hata baada ya kifo cha Mwalimu alikuwa ni Nelson Mandela aliyechukua jukumu la kusaidia kuleta amani Rwanda kama Mpatanishi.

Buriani
Mandela ametutoka baada ya maisha ambayo ametumikia nchi yake, bara lake na dunia kwa namna ambayo ameacha alama ya kudumu ya kukumbukwa. Kwa mtu ambaye utawala wa kikaburu ulimnyima haki nyingi za msingi na kumchukulia miaka ishirini na saba ya maisha yake angeweza kuwa mtu mwenye kisasi pale aliposhika madaraka kama Rais wa nchi yake. Mtu ambaye alinyanyaswa, kuteswa, na kushindwa hata kuhudhuria mazishi ya mamake kwa namna ya kawaida angekuwa ni mtu mwenye kinyongo sana.
Hata hivyo Mandela alionesha huruma na msamaha wa hali ya juu sana. Aliposhika madaraka alihakikisha kuwa watu weupe wanajihisi salama na kuondoa kabisa roho ya kulipiza kisasi hasa kwa watu weusi ambao waliumia sana mikononi mwa weupe kwa karibu miaka 400. Anapoitwa “Baba wa Taifa” la Afrika ya Kusini haitwi hivyo kirahisi. Mchango wake wa pekee kwa nchi yake unamuweka katika nafasi ya pekee kukumbukwa na vizazi vingi vijavyo. Hali hii ya msamaha iligusa hata maisha yake binafsi. Pamoja na kupata habari za mkewe Winnie Mandela kukosa uaminifu Mandela bado alihakikishia kuwa anapatiwa uwakilishi wa kutosha kujitetea kwenye kesi iliyomkabili ya utekaji na mauaji. Hata baada ya kuachana naye Mandela na mkewe mpya Graca Machel – aliyekuwa mke wa marehemu Samora Machel (Rais wa Msumbiji aliyeuawa kwa njama za makaburu) – Mandelea amekuwa na mahusiano mazuri na ya utulivu na Winnie ambaye ameshiriki vilivyo katika kumuuguza Madiba.
Dunia kwa hakika imepoteza shujaa wa haki za binadamu, nyota ya Afrika na mfano wa viongozi ambao waliweka maslahi ya watu wao mbele zaidi kuliko furaha zao binafsi na za familia zao. Wananchi wa Afrika ya Kusini wanapomlilia wanaungana na mamilioni zaidi katika bara la Afrika na Dunia ambao wanakumbuka nafasi ya Mandela katika maisha yao.
Kwa Watanzania wengi hasa waliokua miaka ya sabini na themanini harakati za kutaka Mandela afunguliwe na kukomeshwa kwa utawala wa kikaburu zilikuwa ni sehemu ya maisha yao. Hawa pia wanamshukuru Mungu kwa maisha ya Mandela na wanaungana kutoa rambirambi na pole kwa familia ya Mandela na kumwombea pumziko la amani baada ya maisha ya uchovu na kazi ngumu. Watanzania wanaungana na ndugu zao wa Afrika ya Kusini katika maombolezo haya; wao wenyewe wanakumbuka vile vile jinsi walivyoondokewa na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere na jinsi akili ya jumla ya Taifa ilivyoguswa lakini pia kuonekana kwa kubadilika kwa taifa kwa kutokuwepo Mwalimu. Ni wazi kuwa hata Afrika ya Kusini nayo itapita huku ambapo ile Dhamira ya Taifa (Consciousness of a Nation) yaani Mandela atakuwa hayupo. Njia pekee ya kuhakikisha kuwa Afrika ya Kusini inazidi kujijenga katika maisha ya kisasa na kuinua watu wake kuelekea maendeleo ni lazima kukumbuka umoja na udugu ambao Mandela alipigania.
  Na. M. M. Mwanakijiji

Share this:

 
Copyright © CHIWILEINC. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates