MAHOJIANO YETU NI OVYO KABISAAA



Na edo kumwembe

BADO Napata wakati mgumu. Nafungua magazeti ya Ulaya nayasoma huku natabasamu. Halafu baadaye nafungua magazeti ya nyumbani huku nakunja sura. Na hasa linapokuja suala la mahojiano.
Unasoma kwa makini kauli ya mtu unayemuheshimu. Ukimaliza unakunja sura. Unatamani kupata namba

yake ya simu umepigie na kumuuliza kama kweli ni yeye ndiye aliyeongea au wamemnukuu vibaya. Unakosa namba yake. Lakini siku zinapita mwenyewe hakanushi. Unajua kweli aliongea.
Kiurahisi tu hivi karibuni nilisoma sehemu Mwenyekiti wa Yanga akizungumzia kuhusu Frank Domayo kwenda Yanga. Nilitamani kuamini kuwa alikaririwa vibaya. Alisema “Kuna akina Domayo wengi Kariakoo wanapatikana. Mwache aende tu baadaye atarudi mwenyewe Yanga.”
Hapo hapo unajiuliza kama nafasi hiyo angekuwa anaikalia Ed Woodward wa Manchester United au Florentino Perez wa Real Madrid angeweza kusema “Domayo ni mmoja kati ya viungo bora nchini. Ni pigo kwetu na ni faida kwa Azam, lakini tutakuwa makini kutafuta mbadala wake. Tunamtakia kila la kheri huko aendako kwa sababu ameitumikia vema klabu yetu kwa miaka mitatu iliyopita.”
Nakumbuka Juni mwaka juzi wakati wa mapumziko wa mechi ya Ivory Coast na Tanzania uwanja wa Felix Houphouet-boigny nilimfuata Yaya Toure ambaye hakucheza mechi hiyo kumuuliza kuhusu kiwango cha Taifa Stars. Alinijibu kwa upole “Timu yenu ni nzuri na mnapiga pasi za haraka. Tatizo dogo nililoliona ni kuwa wachezaji wenu hawana nguvu sana. mna wachezaji wowote wanaocheza Ulaya?”
Najaribu kuvuta picha kama Yaya Toure angekuwa Mtanzania, halafu timu yake ya Tanzania ni kama Ivory Coast. Naweza kujibu ambacho angesema. Lazima angesema “Hamna wachezaji nyinyi. Bado hamna uwezo kabisa. Kwanza hamjawahi kushiriki kombe la dunia.”
Unamfuata kocha wa timu kubwa kabisa. Unamuuliza unaionaje Yanga na pambano lenu dhidi yao wiki ijayo. Kocha anajibu “Yanga ni kama mti wa uani. Nikirudi nyumbani napopoa tu nakula. Yaani Yanga ni kama mapambo ya Jeneza tu.” Anayesema hivi ni kocha wa kulipwa ambaye maisha yake yanategemea soka.
Lakini kama Yanga ingekuwa inacheza na Manchester United, Sir Alex Ferguson angejibu kwa umakini mkubwa huku akiwaangalia waandishi usoni. “Tunaiheshimu Yanga kwa kiasi kikubwa. Navutiwa na viungo wao na itabidi tuongeze umakini katika eneo hilo ikiwemo kumdhibiti zaidi Haruna Niyonzima”.
Huyu ni Ferguson ambaye ametwaa mataji ya mawili ya Ulaya. Ametwaa mataji kibao ya Ligi Kuu ya England. Anaheshimika duniani kote. Lakini hapotezi heshima kwa timu yoyote anayocheza nayo.
Amiss Tambwe amefunga mabao 19 msimu ulioisha. Ni mmoja kati ya washambuliaji hatari kwa kuziona nyavu ukanda huu wa Afrika Mashariki na kati. Lakini niliwahi kumsikia kocha mmoja akiulizwa vipi kuhusu Tambwe katika pambano lao linalofuata.
Alijibu kwa haraka haraka “Bwana Kitenge, Tambwe ni mviziaji tu, lakini nakwambia njoo uwanja wa Taifa kesho uone shughuli atakayokumbana nayo.”
Kama kungekuwa na shule kichwani kwake, au upeo mzuri wa kawaida angeweza kujibu “Tambwe ni mmoja kati ya wafungaji tishio nchini na wote tunafahamu hilo. Ni mfungaji wa mfano sana na katika timu yetu tunamuheshimu sana. Lakini nadhani tumejiandaa kupambana vizuri na Simba kwa ujumla na sio Tambwe peke yake. Tutajitahidi kupata pointi tatu kesho.”
Hakuna unachoweza kufanya zaidi ya kucheka tu. Tatizo ni shule au upeo wa kawaida? Rafiki yangu Gaudence Mwaikimba zamani alikuwa anamtungua kipa Juma Kaseja mara nyingi wakutanapo. Hata alipohamia Azam hadithi iliendelea kuwa hiyo hiyo.
Lakini siku moja na yeye akapata bahati ya kuhojiwa kuhusu hilo. Nikasoma katika gazeti. “Kaseja hanisumbui kabisa. Yaani nitamfunga ninavyotaka popote pale tukikutana.”
Hapo hapo unakumbuka mahojiano ya Wayne Rooney wakati alipoulizwa ni kwa nini amekuwa akiifunga Arsenal mara kwa mara tangu akiwa Everton mpaka Manchester United. Alijibu kwa umakini huku akijikuna nywele zake.
“Nadhani ni bahati tu. Mara nyingi inatokea tu kuwa Napata nafasi nzuri na kufunga. Lakini leo nataka kuipongeza timu yetu yote. Tumecheza kwa umakini mkubwa katika mechi hii dhidi ya Arsenal na tumepata pointi tatu muhimu.”
Hawa ndio wenzetu. Wachezaji kama akina Wayne Rooney hawajaenda shule sana. alikuwa na muda gani wa kusoma wakati alisaini mkataba wake wa kucheza soka la kulipwa akiwa na umri wa miaka 15? Tangu hapo ni soka na yeye, yeye na soka.
Nilipokuwa msemaji wa Coastal Union, kitu cha kwanza nilikuwa napenda kuiheshimu timu pinzani. Utashindaje mechi bila ya kujua ubora au udhaifu wa timu pinzani? Unaziponda Simba, Yanga na Azam zenye Domayo, Kipre Tchetche, Tambwe, Niyonzima na wengineo, unamdanganya nani zaidi ya kuwadanganya wachezaji wako?

Share this:

Post a Comment

 
Copyright © CHIWILEINC. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates