MICHEZO - KUELEKEA DAR DERBY OCTOBER 1 KOCHA YANGA AMEONGEA HAYA

KOCHA Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi ameanza kupandisha homa ya pambano la watani wao Simba baada ya jana kujinasibu kuondoka na pointi tatu katika mchezo huo utakaochezwa Oktoba Mosi, Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Mwambusi alisema timu yake haipewi nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo kutokana na kiwango wanachokionesha Simba kwa sasa kwenye mechi za Ligi Kuu lakini amewahakikishia mashabiki wao kuwa lazima washinde.
“Kama kuna watu wanafikiri tutapoteza mechi yetu dhidi ya Simba, Oktoba Mosi wanajidanganya, mashabiki wetu wasiwe na presha tuna wachezaji wazuri kuliko hao wa Simba na muda ukifika kila mtu ataona kitakachotokea Taifa,” alisema Mwambusi.

Pia Mwambusi alisema beki Andrew Vicent ‘Dante’ yupo vizuri hivyo ukuta wao hautapenyeka kirahisi japo itakuwa mechi yake ya kwanza dhidi ya Simba ila kwa kuwa wamejiandaa vya kutosha wamejipanga kushinda.

Mwambusi alisema Dante ana uwezo wa kumdhibiti mshambuliaji mpya wa Simba raia wa Burundi Laudit Mavugo na asilete madhara kwenye lango lao kutokana na umahiri wa nyota wake.

Simba inaongoza katika msimamo wa ligi baada ya kujikusanyia pointi 13 wakifuatiwa na Yanga wenye pointi 10 huku wakiwa nyuma kwa mchezo mmoja baada ya kushuka dimbani mara nne.

Share this:

Post a Comment

 
Copyright © CHIWILEINC. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates