News wasiokua na uraia wajadiliwe


Tanzania  imeitaka jumuiya ya  kimataifa   kujadili  tatizo  la  uwepo wa watu  ambao si raia wa nchi  yoyote ile.

Pendekezo hilo limetolewa siku ya  Jumanne na Waziri wa Mambo ya Nje na  Ushirikiano wa Afrika Mashariki,  Dkt. Augustine Mahiga ( Mb)    katika  mkutano     wa  Kilele wa  viongozi  kuhusu wakimbizi.

Mkutano huo  uliandaliwa na  Rais wa Marekani Barack Obama  kwa  ubia na nchi za  Ethiopia, Jordan, Mexico, Sweden, Canada  na Ujerumani  ambapo nchi  60  zilialikwa,45 kati ya zilizoalikwa ikiwamo   Tanzania    zilitoa ahadi ya  namna moja ama  nyingine. 

Nchi  hizo ni zile ambazo kwa namna moja ama nyingine   zimekuwa zikiwapokea na kuwahifadhi wakimbizi,  zimekuwa nchi za mpito kwa wakimbizi, au zimekuwa  zikitoa misaada   ikiwamo ya  hali na mali pamoja na kuwapatia uraia, ajira na  misaada ya kibinadamu.

Lengo kuu la mkutano  huo wa  viongozi kuhusu wakimbizi lilikuwa ni kwa nchi kutoa ahadi mpya ambazo  kwayo  zitasaidia katika  kuwapatia fursa za ziada  wakimbizi ili  pamoja na mambo mengine kuwapunguzia changamoto zinazowakabili na kuwafanya wajisikie na kujiona  kuwa  nao ni  binadamua kama  binadamu  wengine.

Akizungumza kwa  niaba ya Serikali,   Waziri Mahiga, amesema, Tanzania  kutokana na jiografia ya nchi hiyo  ilivyo imejikuta  mara kwa mara ikiwa ni kimbilio  la wakimbizi kutoka  nchi jirani.

Akawaeleza  washiriki wa mkutano huo, kwamba, suala la  Tanzania  kuwahifadhi  wakimbizi ni la kihistoria na  halikuanza  jana au juzi.

“ Tanzania kutokana na jiografia yake imejikuta  ikiwa ni kimbilio wa watu wanaotafuta salama ya maisha yao. Tumekuwa  tukiwapokea na kuwahifadhi wakimbizi  tangu miaka  ya 60.  Na  tunatekeleza   jukumu hilo kwa kuzingatia sheria  za kimataifa na mikataba ya kimataifa, na sheria zetu za ndani” akasema Mahiga.

 Na kuongeza kwamba, Tanzania itaendelea na jukumu hilo pale itakapopashwa  kufanya   hivyo kwa  kufuata na kuzingatia sheria  za nchi na  sheria za kimataifa.

Share this:

Post a Comment

 
Copyright © CHIWILEINC. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates