DAR ES SALAAM, Tanzania
MAZISHI ya aliyekuwa mwimbaji mahiri wa taarabu wa nchini Mariam
Khamis ‘Paka Mapepe’, yanatarajiwa kufanyika kesho Jumatano, Magomeni Makuti
wilayani Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Mariam (pichani) ambaye hadi anafariki alikuwa ni mwajiriwa wa TOT
Taarab, alimefariki alfajiri ya kuamkia leo kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili,
kifo chake kikitokana na matatizo ya uzazi, ingawa mtoto wake yu salama.
Kwa mujibu wa Baba Mdogo wa marehemu anayetajwa kwa jina
moja la Sembuli, alisema kuwa, wamefikia uamuzi wa kumzika marehemu kesho, baada
ya kuombwa na Mkurugenzi wa TOT Kapten Komba kufanya hivyo ili wapate
kuhudhuria mazishi ya mfanyakazi mwenzao.
Kundi la taarabu la TOT, liko mjini Dodoma kwa hivi sasa
kwenye Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), ambapo msiba wa marehemu huko
nyumbani kwa baba yake mkubwa Magomeni Makuti, Mtaa wa Ndovu Bar,
yanakotarajiwa kufanyika mazishi hayo.
Mariam Khamis alitamba sana
na wimbo wa Mapaka Mapepe alouimba akiwa na Melody, kiasi cha kumpa jina hilo la utani, kabla ya
kujiunga na Zanzibar Stars, kisha Five Stars na hatimae TOT.
Wimbo wake wa kwanza kurekodi na TOT ulikuwa ni ‘Sidhuriki
na Lawama’ ambao unatamba sana
hadi sasa anapopchukuliwa na mauti yaliyoelezwa kutokana na Kifafa cha Uzazi
alichokumbana nacho baada ya kujifungua kwa operesheni kubwa.
Wasanii mbalimbali wa muziki nchini, hususani wa Taarabu,
wameelezea kustushwa na kifo cha Mariam, ambapo Habari Mseto ulishuhudia
waimbaji na mashabiki mbalimbali kwenye Hospitali ya Muhimbili, ulikohifadhiwa
mwili wa marehemu.
Post a Comment