Tumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametuwezesha kuonana tena wiki hii
tukiwa wazima. Lakini pia tumshukuru kwa kutuletea kitu kinachoitwa
mapenzi.
Mapenzi yamekuwa yakichukua nafasi kubwa sana katika
maisha yetu ya kila siku na yamekuwa yakichangia kwa kiasi kikubwa
furaha kwa kila mtu.
Kama huamini, angalia wale waliotokea
kupenda na wao wakapendwa, utabaini nyuso zao zimetawaliwa na furaha
isiyo na kifani. Lakini mapenzi hayo hayo yamekuwa ni chanzo cha vilio
kwa baadhi ya watu.
Mpenzi msomaji wangu, kupenda hakuna macho!
Moyo ukishapenda hausikii la kuambiwa. Katika hili ndiyo maana unaweza
kumuona mwanaume kazimika kwa demu ambaye hawaendani kabisa lakini moyo
wake ndiyo umeshapenda.
Ilishawahi kutokea msichana akampenda
kijana mmoja ambaye ni fukara kupita maelezo. Yeye akawa ndiyo
anamhudumia kwa kila kitu. Akamfanyia mpango wa ajira na mwisho wake
wakafunga ndoa.
Sasa hivi wanaishi maisha ya furaha na amani.
Wamegeuka mfano wa kuigwa kwa jinsi wanavyopendana lakini huko nyuma
msichana huyo alikuwa akichekwa kwa kutoa penzi kwa mwanaume asiye na
mbele wala nyuma.
Hayo ndiyo mapenzi jamani! Lakini pia katika
kufurukuta kumtafuta mpenzi wa kuwa naye maishani, mwanaume anaweza
kujikuta unaangukia kwa demu ambaye tayari ana mpenzi wake.
Moyo wako unakuambia yeye ndiye mtu sahihi katika maisha yako lakini tayari ana mtu wake, unafanyaje?
Utapambana kuhakikisha unapata kile ambacho moyo wako umekipenda au
utakubaliana na ukweli kwamba huwezi kuwa naye kwa kuwa ana mtu wake?
Inapofikia hatua hiyo unaweza kujikuta upo njia panda hasa pale ambapo
huyo mwenye mtu wake naye anaonesha kuwa na chembechembe za mapenzi
kwako.
Kuna mambo kadhaa ya kukusaidia kukabiliana na hali hii.
Chunguza
Tumia muda wako mwingi kuchunguza juu ya uhusiano wake. Uhusiano wao
umesimama na wanaonekana ni watu wenye ‘future’? Nasema hivyo kwa
sababu, yawezekana uhusiano wa huyo uliyetokea kumpenda ni wa kuzuga tu
na huenda wewe ndiye mwenye ‘future’ naye. Ndiyo maana nikasema chunguza
uhusiano wake kwanza.
Usitafute uadui
Baada ya kuchunguza,
ukibaini kwamba uhusiano wao hauko ‘siriasi’, vuta subira, lolote
linaweza kutokea na likaufurahisha moyo wako. Lakini kama utaona ni watu
walio siriasi na wanaelekea kuoana, usitafute uadui bure, kaa pembeni.
Una nafasi kwake?
Sawa umetokea kumpenda msichana aliye na mtu wake, umeshawahi kujiuliza
kama una nafasi ndani ya moyo wake? Anaonesha dalili fulani za
kukupenda kama unavyompenda na ni mtu anayeonesha kukumisi anapokuwa
mbali na wewe? Utakapobaini una nafasi kwake, uamuzi wa kumpotezea
hautakuwa na nafasi.
Ni rahisi kubadili uamuzi wake?
Unadhani huyo uliyetokea kumpenda anaweza kubadili maamuzi ya kumuacha
huyo aliyenaye kama kweli hawana ‘future’? Utagundua hilo kwa kuongea
naye na kumsikia kama anaweza kufanya maamuzi hayo ili awe na wewe.
Pingana na moyo wako
Ifike wakati upingane na moyo wako. Unajua moyo wako kukuambia kuwa
unataka kuwa na uhusiano na demu ambaye tayari ana mpenzi wake wakati
mwingine utakuwa unakupotosha.
Kwa hiyo ukiona vipi, pingana
nao. Acha kumng’ang’ania msichana mwenye mpenzi wake licha ya ukweli
kwamba, huenda wewe ndiye mwenye nafasi ya kuwa mume wake na siyo huyo
aliye naye.
Urafiki ni poa?
Umempenda sana na hauko tayari
kumkosa katika maisha yako lakini imetokea kwamba tayari yuko na mtu na
umebaini huna nafasi kwake kabisa? Usiumie, omba angalau urafiki. Siyo
urafiki wa kivile sana ila angalau pale unapotaka kusikia sauti yake kwa
kumsalimia tu, upate nafasi hiyo.
Usiumie, yupo mwingine
Haina haja ya kujitafutia vidonda vya tumbo bure kwa kuwa tu umebaini
uliyetokea kumpenda tayari ana mtu. Chukulia ni hali ya kawaida, mademu
wazuri ambao wanaishi singo wapo kibao huko mtaani, ni suala la wewe
kutulia tu. Amini yupo mwingine ambaye atayafanya maisha yako yawe ya
furaha.
Naomba nihitimishe kwa kusema kwamba, unapotokea
kumpenda mtu fulani, pambana kuhakikisha unampata kwa sababu ukimkosa
maisha yako yanaweza kuwa gizani. Ila pale utakapoona uwezekano wa kuwa
naye haupo, usilazimishe ndugu yangu. Kumbuka haya ni maisha tu!
Post a Comment