MAAJABU yameibuka kwenye mazishi ya baba mzazi wa Mtangazaji wa Kipindi
cha Wanawake Live kinachorushwa hewani na Televisheni ya East Africa,
Joyce Kiria, Michael Francis Iwambo Kiria kufuatia kuchimbwa kwa
makaburi mawili, Amani lina mkasa mzima.
Kondoo akichinjwa.
Tukio hilo la ajabu lilitokea kwenye msiba wa mzee huyo, Kata ya
Kibosho, Kijiji cha Dakau, mkoani Kilimanjaro wakati wa maandalizi ya
kuuhifadhi mwili wa merehemu huyo.
Mzee Kiria alifariki dunia Julai 10, mwaka huu jijini Tanga alikokuwa akiishi na mke mwingine (si mama’ke Joyce) baada ya kuugua ghafla.
KWA NINI MAKABURI MAWILI?
Ilielezwa kwamba ndugu wa mzee Kiria waliopo kijijini Dakau walipopata taarifa za kifo cha mzee huyo na kwamba mwili wake utazikwa kijijini hapo walichimba kaburi kwenye eneo la makaburi ya ukoo.
“Maiti ilifika kijijini, taratibu za ibada zilifanyika kanisani, lakini kazi ikawa kwenye kuupeleka mwili kaburini. Mke wa marehemu aliyekuwa akiishi naye Tanga aliuliza eneo lililochimbwa kaburi na kuambiwa ni la ukoo, akasema haiwezekani azikwe hapo.
“Mwanamke huyo alisema marahemu wakati wa uhai wake aliagiza akifa azikwe kwenye shamba alilopewa na baba yake mzazi, mzee Francis Kiria na si vinginevyo,” alisema mpashaji wetu aliyekuwa eneo la tukio.
MSIBANI HAPAKALIKI
Vuta nikuvute ilitokea eneo la msiba, mke wa marehemu aliweka wazi msimamo wake kwamba endapo ndugu watalazimisha marehemu azikwe eneo la familia angeondoka na maiti kurudi nayo Tanga kwa mazishi.
JOYCE KIRIA AMWAGA MACHOZI, APIGA MAGOTI
Ilibidi ndugu waweke kikao cha dharura cha familia ili kumshawishi mwanamke huyo akubaliane na matakwa ya familia kwa sababu ndugu wote walizikwa makaburi ya ukoo, lakini mjane huyo alitia ngumu.
“Yule mke wa marehemu alikataa katakata, alisema lazima mume wake azikwe kwenye shamba alilopewa na baba yake kama alivyotaka akiwa hai.
“Ilifika mahali, Joyce Kiria alimpigia magoti mwanamke huyo huku akilia na kumuomba aruhusu baba yake azikwe kwenye kaburi lililokwisha chimbwa kwenye eneo la ukoo, lakini wapi, mwanamke aligoma,” alizidi kusema mpashaji wetu.
KABURI LA PILI LACHIMBWA
Kwa mujibu wa mtoa habari wetu, baada ya msimamo wa mwanamke huyo kusimama kwenye maamuzi, ilibidi ndugu wakubaliane naye kwa kutuma watu kwenda kuchimba kaburi la pili kwenye shamba la marehemu.
Cha ajabu, wakati wachimbaji wakiendelea na zoezi hilo, kondoo mmoja mweupe alianza kulia kwa muda mrefu jambo lililowashangaza watu walioshuhudia.
Wengi wa watu hao walihoji kilio cha kondoo huyo wakisema huenda aliashiria mambo fulani ambayo wazee wa kimila ndiyo wanatakiwa kufuatilia na kutoa ufafanuzi.
Mbali na kilio cha kondoo huyo, baadhi ya watu walisikika wakisema wanaamini baada ya mazishi hayo, kifo kingine kitajiri kwa sababu haijawahi kutokea kijijini hapo makaburi yakachimbwa mawili kwa ajili ya marehemu mmoja.
WAZEE WA KIMILA WAKAA KIKAO
Kufuatia kuwepo kwa makaburi mawili, habari zinasema ilibidi wazee wa kimila kuketi kikao cha ghafla na kuulizana mila na desturi za mababu ni nini inapotokea hali kama hiyo.
Ndipo mzee mmoja alisema lazima kondoo mmoja mweupe achinjwe kisha damu yake kumiminiwa ndani ya kaburi lisilotakiwa halafu mzoga wa kondoo huyo ufukiwe katika kaburi.
Kondoo aliyepata ‘kura nyingi’ ni yuleyule aliyelia baada ya mjane wa marehemu kushinda eneo la kuzikiwa mume wake.
KONDOO AKAMATWA, ASOGEZWA KABURINI, ACHINJWA
Kondoo huo alikamatwa, akasogezwa jirani na kaburi, akachinjwa mpaka kukata roho. Damu yake ilimiminikia kaburini, nyingine ilikingwa kwenye kikombe na kumiminiwa kaburini halafu mzoga wake ukatupwa humo na kufukiwa.
BABA WA JOYCE AZIKWA SASA
Baada ya kufanyika kwa mambo hayo yote, mwili wa marehemu ukiwa ndani ya jeneza la mbao lenye rangi ya damu ya mzee ulipelekwa kuzikwa kwenye kaburi lililochimbwa shambani kwake.
Mazishi yalifanyika kwa amani, baadaye waombolezaji walitawanyika kurudi eneo la msiba lakini gumzo kuu likiwa kuchinjwa na kuzikwa kwa kondoo huyo.
Baadhi ya watu kijijini hapo wenye rika la utu uzima, walisikika wakisema hawajahi kuona mnyama akitolewa kafara ya kifo cha binadamu.
Wengi walisema wanachokijua wao ni kwamba, utata wa kaburi humalizwa kwa kuzikwa mgomba au majani yaitwayo isale.
JOYCE KIRIA ANENA
Baada ya kupata habari hiyo ya kusisimua, juzi Amani lilimtafuta Joyce Kiria ili kuthibitisha kutokea kwa habari hiyo na kumpata nyumbani kwake, Changanyikeni, jijini Dar ambapo alikiri na kusema hata yeye mwenyewe haelewi kitu ambacho kimetokea kwa sababu hajawahi kuona katika maisha yake.
“Kwa kweli hayo ni majaabu kwangu, hata mimi nimeshangaa kupita kiasi, sijawahi kuliona jambo hili katika maisha yangu na limeniumiza kupita kiasi,” alisema Joyce huku machozi yakimlengalenga.
Mungu ailaze pema peponi roho ya marehemu Michael Kiria.
Post a Comment