Na Issa Mnally
MIEZI nane baada ya kufariki dunia mumewe Juma Kilowoko ‘Sajuki’, ...
hatimaye mume wa pili wa staa wa filamu za Kibongo, Wastara Juma
aitwaye Ahmed Kushi ameibuka na kudai kwamba anatambua kwamba staa huyo
bado ni mkewe na anataka ampatie mwanaye aliyezaa naye.
Kwa muda mrefu kulikuwa na taarifa kuwa Wastara aliachana na mwanaume
huyo kwa talaka kabla ya kuolewa na Sajuki lakini kuibuka kwake na
madai kuwa bado mwanadada huyo ni mkewe kumezua mshangao mkubwa.
MADAI YA KUSHI
Alisema: “Kisheria bado ni mke wangu kwa kuwa nilikuwa nimempa talaka moja tu wala hazikufika tatu,”
alisema Kushi na kudai kwamba ndoa yake na staa huyo ilidumu kwa mwaka
mmoja na nusu na kuvunjika kutokana na kutawaliwa na migororo.
Jamaa huyo alidai kuwa zaidi ya mara tatu amekuwa akimtaka Wastara
ampatie mwanaye huyo ambaye kwa sasa ametimiza miaka minane bila ya
mafanikio.
KWA NINI WAKATI HUU?
Gazeti hili liliamua kumbana kwa kumuuliza kwa nini ameibuka wakati
huu baada ya Sajuki kufa na mbona hakujitokeza kwa zaidi ya kipindi cha
miaka kumi iliyopita? Pia akaulizwa kwa nini ameamua kutafuta umaarufu
kwa kumdhalilisha? Akaishia kukaa kimya.
WASTARA AFUNGUKA
Baada ya Kushi kuibuka na ishu hiyo yenye utata, gazeti hili lilizungumza na Wastara ambapo alikuwa na haya ya kusema:
“Kuhusu mtoto, kama kweli alikuwa na
lengo la kumchukua mwanaye na ananijua, basi atakuwa anawajua wazazi
wangu hivyo angefuata utaratibu.
“Hakuna utaratibu kama huo kama kweli
anamhitaji mwanaye angeenda kwa wazazi wangu, huko ni kunidhalilisha kwa
kuwa ananiona mnyonge baada ya kufiwa na mume wangu Sajuki.
“Kama siyo kunidhalilisha ni nini?
Naomba asitumie jina langu kutafuta umaarufu kwa kunichafua. Naomba
aache kwa sababu ananiongezea maumivu juu ya maumivu.”
Kuhusu madai kwamba bado ni mkewe, Wastara alilia: “Hivi
huyo mtu alikuwa wapi muda wote nikiwa na Sajuki? Mbona hakuibuka
wakati mume wangu akiwa hai? Najua anatumia kigezo cha kuondoka Sajuki
kunionea lakini Mungu anajua.”
NI KWELI ALIFUNGA NDOA NA KUSHI?
Pamoja na kumbembeleza aeleze kama kweli aliwahi kufunga ndoa na Kushi, Wastara alisema: “Sitaki kumzungumzia mtu, naomba watu wawe na huruma kwangu, wasitumie kigezo cha kumpoteza Sajuki kunidhalilisha.”
SHEHE AMPINGA KUSHI
Gazeti hili halikuishia hapo, lilimtafuta shehe wa Msikiti wa Nuur wa
Magomeni-Mapipa jijini Dar, Juma Simba ili kupata ufafanuzi juu ya
talaka moja ambapo alimpinga Kushi kwa kusema kuwa kisheria Wastara si
mkewe tena.
“Kumpa talaka moja si sababu ya
kuendelea kuwa mke wake mpaka leo hii, sheria inasema kuwa Kushi
alitakiwa kumrejea Wastara kabla ya miezi mitatu kupita tangu alipompa
talaka moja,” alisema na kusisitiza kuwa ndoa hiyo ilishakufa.
YATOKANAYO
Awali ilidaiwa kuwa Wastara aliwahi kuolewa mara mbili kabla ya kufunga ndoa na staa mwenzake wa filamu, Sajuki.
Ndoa ya kwanza ya Wastara aliifunga mwaka 1998 na Juma Mpemba ambaye alibahatika kupata naye mtoto mmoja wa kiume aitwaye Samir.
Sajuki alikuwa mume wa tatu kwa Wastara ambaye naye alibahatika kupata mtoto mmoja wa kike aitwaye Farheen.
Chanzo:Global Publisher Blog
Post a Comment