Home
»
Makala
» MAKALA YA EDO KUMWEMBE
MAKALA YA EDO KUMWEMBE
By
Unknown
•
4:37 AM
•
Makala
•
Diamond na Ngassa nao watalia?
NA EDO KUMWEMBE
MACHOZI yanawalengalenga. Ni huzuni. Watu mashuhuri katika fani wote
wanalalamika. Jellah Mtagwa analalamika, Maalim Gurumo analalamika,
Rashida ‘Snake Boy’ Matumla analalamika. Wote machozi yanawatoka.......
Wote wanahisi wanaishi katika umaskini tofauti na umashuhuri wa zama
zao. Kila mmoja anahisi dunia imemtupa katika shimo la takataka.
Hawawaoni tena wale mashabiki waliokuwa wanawazunguka kwa macho ya
husuda wakati ule walipokuwa katika ubora wao.
Jellah, mmoja kati ya
walinzi bora kuwahi kucheza katika nyasi za viwanja vyetu analia na
umaskini huku maradhi ya kupooza yakimsumbua. Huyu ni Mwanasoka ambaye
mwaka 1982 picha yake iliwekwa katika stempu za Shirika la Posta nchini.
Maalim Gurumo ameimba muziki kwa miaka 50. Sasa hivi miguu inamuuma na
pesa ya tiba inamsumbua. Gari lake la kwanza maishani amepewa na
mwanamuziki wa kizazi kipya, Diamond Platinum ambaye ameanza kuimba
muziki katika Utawala wa Rais Jakaya Kiwete.
Katika sura iliyonuna
na isiyotaka masikhara ya Rais wa awamu ya tatu, Ben Mkapa, bado Rashid
Matumla aliitwa Ikulu kupeleka mkanda wake wa dunia kutokana na makali
yake ya wakati huo.
Lakini sasa kila kitu kinakwenda kombo. Kuna
kila dalili kwamba Serikali inaingizwa lawamani na mashabiki au wahusika
wenyewe kwa kile kinachoonekana kutowajali mastaa wa zamani ambao
wanatajwa kuwa walilitumikia na kulipa sifa taifa.
Siwezi kuzuia
vilio. Lakini nataka tufunuane ubongo. Kuna sehemu ambayo tumekosea,
tunakosea, na tunaendelea kukosea. Watanzania walio katika fani
mbalimbali wamekosa ujasiri na uthubutu wa kufuata misingi ya sera ya
Kibepari inavyohitaji.
Sera za kibepari (Capitalism) ingawa
hazisemi wazi lakini zinamtaka mwanadamu awe mbinafsi katika maisha yake
ya kila siku na awe makini katika kujijali mwenyewe kwa umakini mkubwa
pamoja na Familia yake.
Ni katika Ujamaa tu ndipo ambapo mtu anaishi
kwa ajili ya watu wengi waliomzunguka, pamoja na Serikali yake.
Wanamichezo wetu na wasanii wamelala katika dunia ya zamani.
Wamelala katika dunia iliyowaaminisha kwamba wao ni wasanii au
wanamichezo wa serikali pamoja na wananchi wake. Matokeo yake, matatizo
mengi yanayowatokea katika siku za usoni wanayalaza katika mikono ya
Serikali pamoja na Wananchi.
Kwa mfano, Mwanamuziki hapaswi kuimba
bure katika shughuli yoyote ya Chama na Serikali kwa ajili ya upendo
wake. Muziki ni biashara na ni kazi kama zilivyo nyingine. Kuachana na
ubinafsi wa Kipato kwa kujali Sherehe za Mwenge wa Uhuru ni kujiandalia
njia za umaskini wa baadae.
Kwa wenzetu, kuichezea timu ya taifa
kama Jellah alivyofanya enzi zake kunaambatana na mambo matatu. Kwanza
ni Uzalendo kwa taifa. Pili ni kuongeza kipato cha pesa, tatu ni
kuongeza wasifu (CV) kwa mawakala na macho ya Mameneja wa mchezo huo.
Hili la tatu ni kubwa kwao. Lakini kama unacheza kwa ajili ya
kuifurahisha Serikali au Mashabiki waliojitokeza uwanjani, unafanya kosa
kubwa la kiufundi katika dunia ya kibepari.
Jaribu kumtazama Rashid
Matumla katika ubora wake. Kiwango alichofikia kilimaanisha kwamba
Rashid ilikuwa lazima awe na kundi la Wasomi lililomzunguka kwa ajili ya
kuendesha jina lake na kulitanua zaidi katika masoko, Matangazo na
dunia ya kibiashara ya ngumi.
Ni kwa namna gani alifanya juhudi
kuhakikisha hilo? Ni kwa kiasi gani washauri wake walifanya juhudi za
kumpeleka Rashid katika anga za Floyd Mayweather, Manny Pacquiao, David
Haye na wengineo?
Je kosa alilolifanya Rashid wakati huo, hatuoni
kama ni kosa ambalo leo Francis Cheka analirudia? Na wakati ukifika,
tutalazimika kuingia katika mkumbo wa kusikiliza kilio cha Cheka na
umaskini wake wa wakati huo?
Watanzania tumelala katika dunia yetu
peke yetu. Sera za Ujamaa wakati Fulani huwa zinatugharimu kwa sababu
tunaamini kuwa mwanadamu yupo kwa ajili ya kuifanyia kazi na
kuiburudisha Jamii inayomzunguka. Hatuamini kwamba mwanadamu inabidi uwe
mbinafsi na kuitumia fursa aliyonayo kwa ajili ya maslahi yake binafsi
na ya watoto wake hili mradi usiwe Mwizi au tapeli.
Leo Mike Tyson
amefilisika. Hakuna anayemlilia zaidi ya kujililia mwenyewe. Sijasikia
akimlaumu Barrack Obama na Serikali yake. Sijasikia akiilaumu Serikali
ya Marekani.
Leo, Paul Gascoigne Gazza amefilisika na amejikita
katika ulevi uliotopea. Sijamsikia Gazza akiilaumu FA wala viongozi wa
timu alizopitia. Anajua kwamba wakati anacheza soka aliishi maisha yake
na aliyatawala maisha yake kwa namna alivyojisikia.
Unaposikia
mchezaji yupo katika maongezi ya kuongeza mkataba wake huku maongezi
hayo yakichukua zaidi ya miezi sita ni kwa sababu anatetea maisha yake
ya uzeeni. Anajua atastaafu mwenyewe, ataishi mwenyewe, atajifia
mwenyewe.
Ni nani atakubali kusikiliza kilio cha Diamond Platinum
wakati akiwa amechoka? Ni nani atakubali kusikia kilio cha Mrisho Ngassa
na ofa alizopata maishani? Wakati wao ni huu na ndio muda wa
kutengeneza pesa na kuwekeza katika miradi ya kudumu. Serikali na
mashabiki tutaingiaje katika kilio cha wakati huo?
Serikali ni nini
hasa? Ni muundo tu wa kiutawala dhidi ya Wananchi. Lakini wanaotawala
ndani ya serikali ni binadamu kama sisi. Nao wanakufa, wanabadilika
madarakani, na wenyewe pia wana matatizo yao kibao. Ukiililia serikali
unamlilia nani hasa?
Tuanze kubadili mtazamo. Waliokosea walikosea,
lakini tusiruhusu waliopo wapotee zaidi. Unaimbaje bure katika sherehe
ya Serikali? Kwanini unaruhusu Ringtone za simu zijae nyimbo zako bure?
Kwanini ukatae ofa ya mshahara wa dola 5,000 kutoka El Marreikh?
Kwanini usikubali kuwa chini ya uangalizi wa kampuni yoyote makini
ambayo una mkataba nao wa kisheria? Na kwanini mpaka leo usiwe na
Mwanasheria au mshauri wako wa masuala ya kazi zao katika mwelekeo wa
kibiashara.
SIMILAR ARTICLES
Post a Comment