Home
»
Makala
» MAKALA NA EDO KUMWEMBE
MAKALA NA EDO KUMWEMBE
By
Unknown
•
3:40 AM
•
Makala
•
NA EDO KUMWEMBE
WAKATI mwingine hakuna unachoweza kufanya zaidi ya kucheka. Hata kama
haucheki usoni. Unacheka moyoni na kujiuliza, ni namna gani Kigogo
anayehusika na wizi wa Meno wa Tembo anavyokandia uwezo wa Mrisho
Ngassa.
Ndio, unakutana na Mbunge Kigogo. Jina lake linatajwa katika
wizi wa Meno ya Tembo. Anakwambia “Hivi Edo unataka kuniambia niache
kushangilia Manchester nije kutazama Taifa Stars. Hatujui mpira sisi
Watanzania”. Moyoni namjibu, kweli hatujui mpira, lakini kulinda
Rasilimali zetu kama Meno ya Tembo unayoiba ndio tumeweza?
Unajiuliza, sawa sisi hatujui mpira, lakini tumefanikiwa katika nini
hasa? Barabara? Madini? Kilimo? Siasa? Elimu? Hapana. Hatimaye tumefika
katika nyakati ambazo Taifa kama Taifa limekwama. Ni kitu gani kingine
cha kujivunia wakati unapoponda soka la Tanzania? Hakuna.
Aliyempa
tenda mkandarasi mbovu kujenga barabara mbovu ya Kilwa, naye anauponda
mpira wa Tanzania. Aliyesaini mkataba mbovu wa Madini ambao unaruhusu
Mzungu kuchota Madini yetu atakavyo, naye anamponda kocha wa Taifa Stars
na wachezaji wake.
Anayeongeza sifuri katika hesabu ya safari za
Rais Ulaya naye akikutana na Watanzania wanaoshi nje anauponda mpira wa
Tanzania. Yeye ni Mwizi mzuri tu, lakini wala haoni hesabu za wizi wake
zinavyoshindwa kusomesha walimu wa soka nje ya nchi.
Umewahi
kumsikia Mbunge wa kile Chama akiponda wachezaji wa Tanzania? Lakini
ndiye huyo huyo aliyegonga meza na wenzake kupitisha bajeti ya Wizara ya
Elimu na Michezo na wakaipa shilingi 600 milioni. Huo ni mshahara wa
wiki moja wa mchezaji anayetoka nchi ya Afrika anayecheza Ulaya, Yaya
Toure. Bajeti hii ya mshahara wa wiki wa Yaya Toure inainuaje soka?
Anayepaswa kutatua tatizo la foleni jiji la Dar es salaam akashindwa na
kujiongezea posho za kijinga kila siku naye analaumu matokeo mabovu ya
timu ya Taifa na viwango vibovu vya Simba, Yanga, Azam katika michuano
ya Caf.
Kigogo wa TRA ni shabiki mzuri wa Arsenal. Anamsaidia yule
Mfanyabiashara maarufu kukwepa kodi. Hajui kwamba pesa tunayopoteza
ingesaidia uchumi wa nchi na michezo wa ujumla. Hapa huwa ananiacha hoi
kweli kweli.
Lakini anauchekaje mchezo wa soka? Kama mchezo wa soka
umefeli, kwani hajui ni kwa kiasi gani Tanzania imefeli katika kukusanya
kodi nyingi miongoni mwa nchi za Afrika? Hapa si ndio nchi ambayo
Mfanyabiashara anapewa miaka mitano ya kutolipa kodi mpaka ajue faida ya
biashara yake? Wenyewe wanaita kwa kizungu Tax Holiday.
Kigogo wa
Wizara nyeti ya ulinzi anamlinda Kigogo mwenzake aliyebaka mtoto wa
kiume. Wakiimaliza kesi kituo cha Polisi wanaitana Serena Hoteli
kupongezana kwa kula mishkaki huku wanacheki mechi ya Taifa Stars dhidi
ya Ivory Coast TBC. Tukifungwa wanasema hatujui mpira na wachezaji wetu
ni duni.
Unajiuliza, kwani mchezaji wa Tanzania si anatokana na
mtoto wa Kitanzania? Mbona wametoka kumkandamiza mtoto wa Kitanzania?
Naishia kucheka taratibu kwa uchungu.
Mchezaji mwenye kipaji kama
Haruna Moshi ‘Boban’ hajaweza kung’ara Ulaya. Kuna tofauti gani na Mlima
Kilimanjaro kushindwa kusaidia uchumi wa Taifa lake zaidi ya ilivyo
sasa. Kuna tofauti gani na Mtanzania kufa njaa wakati ana ardhi kilomita
nyingi zenye rutuba?
Mwisho wa yote tunaishi katika Taifa
lililooza. Taifa lisilo na maadili katika uchumi, jamii na siasa. Kila
unapowaza unakubali kwamba soka la Tanzania lipo chini na limeoza.
Hatuonyeshi matumaini. Lakini niambieni ni wapi kuna matumaini na
nidhamu?
Tatizo limebaki kwa Mtanzania mwenyewe. Hana uzalendo,
ubunifu na umakini. Niambieni ni nani halaumiwi? Mwandishi wa habari?
Mchezaji? Polisi? Rais? Mbunge? Mwanajeshi? Daktari? Mmachinga?
Mfanyabiashara? Mkulima? Kila mtu haifanyi kazi yake sawa sawa.
Ni
kweli. Tumekosa dira kama taifa. Hatujui tulipo wala tunapokwenda. Kabla
haujamlaumu mwenzako jiulize, wewe unaifanyia nini nchi yako. je wewe
Sekta yako ina maendeleo yanayostahili kabla ya kumnyooshea kidole
mwingine?
Huwa nawaza sana. Daktari aliyemfanyia operesheni ya
kichwa mtu anayestahili kufanyiwa operesheni ya goti, naye anamlaumu
Polisi aliyechukua rushwa jana Kariakoo. Na yule polisi naye analaumu
matokeo mabovu ya timu ya taifa. Na hata wachezaji wa timu ya taifa
wanalalamika kuwa Rais anaendesha nchi hovyo. Rais naye ana malalamiko
yake mengi kwa wananchi wa Mtwara kukataa gesi kutoka kusini.
kila
mtu anamlaumu mwingine. Cheni ya lawama inakuwa ndefu, lakini mwisho wa
siku ukweli unabakia pale pale kwamba Taifa limekosa maadili. Nani yuko
salama na nani anafanya kazi yake kwa maadili makubwa?. Hakuna.
Kigogo anayeongoza Bandari anajifanya analaumu kwanini wachezaji wa
Tanzania hawachezi Ulaya. Wala hajiulizi kwanini chini ya Bandari yake
uchumi wa Tanzania usiongoze Afrika Mashariki na kati na baadhi ya nchi
za Ulaya zisizo na Bandari.
Wabrazil wanakosea kwingine, lakini
mpira wanajua. Wachina wanakosea katika mpira, lakini uchumi wanajua.
Wamarekani wanakosea katika moja kidogo, lakini jingine wanafahamu.
Ethiopia wana umaskini, lakini katika riadha wanapatia. Katika soka
wanajitokeza.
Tanzania tunafahamu nini zaidi? Tumepatia wapi hadi
tuseme mpira ni tatizo sana? wasomi na wananchi wa kawaida tuanze
kuitafakari nchi kwa pamoja. Tusitafakari kwa mapande mapande. Tuna
tatizo kila sehemu. Nani hajawahi kulaumiwa au kulaumu? Kila mtu tatizo
nchi hii…
SIMILAR ARTICLES
Post a Comment