Tanzania imeitaka jumuiya ya kimataifa kujadili tatizo la uwepo wa watu ambao si raia wa nchi yoyote ile.
Pendekezo hilo limetolewa siku ya Jumanne na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga ( Mb) katika mkutano wa Kilele wa viongozi kuhusu wakimbizi.
Mkutano huo uliandaliwa na Rais wa Marekani Barack Obama kwa ubia na nchi za Ethiopia, Jordan, Mexico, Sweden, Canada na Ujerumani ambapo nchi 60 zilialikwa,45 kati ya zilizoalikwa ikiwamo Tanzania zilitoa ahadi ya namna moja ama nyingine.
Nchi hizo ni zile ambazo kwa namna moja ama nyingine zimekuwa zikiwapokea na kuwahifadhi wakimbizi, zimekuwa nchi za mpito kwa wakimbizi, au zimekuwa zikitoa misaada ikiwamo ya hali na mali pamoja na kuwapatia uraia, ajira na misaada ya kibinadamu.
Lengo kuu la mkutano huo wa viongozi kuhusu wakimbizi lilikuwa ni kwa nchi kutoa ahadi mpya ambazo kwayo zitasaidia katika kuwapatia fursa za ziada wakimbizi ili pamoja na mambo mengine kuwapunguzia changamoto zinazowakabili na kuwafanya wajisikie na kujiona kuwa nao ni binadamua kama binadamu wengine.
Akizungumza kwa niaba ya Serikali, Waziri Mahiga, amesema, Tanzania kutokana na jiografia ya nchi hiyo ilivyo imejikuta mara kwa mara ikiwa ni kimbilio la wakimbizi kutoka nchi jirani.
Akawaeleza washiriki wa mkutano huo, kwamba, suala la Tanzania kuwahifadhi wakimbizi ni la kihistoria na halikuanza jana au juzi.
“ Tanzania kutokana na jiografia yake imejikuta ikiwa ni kimbilio wa watu wanaotafuta salama ya maisha yao. Tumekuwa tukiwapokea na kuwahifadhi wakimbizi tangu miaka ya 60. Na tunatekeleza jukumu hilo kwa kuzingatia sheria za kimataifa na mikataba ya kimataifa, na sheria zetu za ndani” akasema Mahiga.
Na kuongeza kwamba, Tanzania itaendelea na jukumu hilo pale itakapopashwa kufanya hivyo kwa kufuata na kuzingatia sheria za nchi na sheria za kimataifa.
Post a Comment