MAKALA NA EDO KUMWEMBE

NA EDO KUMWEMBE
WAKATI mwingine hakuna unachoweza kufanya zaidi ya kucheka. Hata kama haucheki usoni. Unacheka moyoni na kujiuliza, ni namna gani Kigogo anayehusika na wizi wa Meno wa Tembo anavyokandia uwezo wa Mrisho Ngassa.
Ndio, unakutana na Mbunge Kigogo. Jina lake linatajwa katika wizi wa Meno ya Tembo. Anakwambia “Hivi Edo unataka kuniambia niache kushangilia Manchester nije kutazama Taifa Stars. Hatujui mpira sisi Watanzania”. Moyoni namjibu, kweli hatujui mpira, lakini kulinda Rasilimali zetu kama Meno ya Tembo unayoiba ndio tumeweza?
Unajiuliza, sawa sisi hatujui mpira, lakini tumefanikiwa katika nini hasa? Barabara? Madini? Kilimo? Siasa? Elimu? Hapana. Hatimaye tumefika katika nyakati ambazo Taifa kama Taifa limekwama. Ni kitu gani kingine cha kujivunia wakati unapoponda soka la Tanzania? Hakuna.
Aliyempa tenda mkandarasi mbovu kujenga barabara mbovu ya Kilwa, naye anauponda mpira wa Tanzania. Aliyesaini mkataba mbovu wa Madini ambao unaruhusu Mzungu kuchota Madini yetu atakavyo, naye anamponda kocha wa Taifa Stars na wachezaji wake.
Anayeongeza sifuri katika hesabu ya safari za Rais Ulaya naye akikutana na Watanzania wanaoshi nje anauponda mpira wa Tanzania. Yeye ni Mwizi mzuri tu, lakini wala haoni hesabu za wizi wake zinavyoshindwa kusomesha walimu wa soka nje ya nchi.
Umewahi kumsikia Mbunge wa kile Chama akiponda wachezaji wa Tanzania? Lakini ndiye huyo huyo aliyegonga meza na wenzake kupitisha bajeti ya Wizara ya Elimu na Michezo na wakaipa shilingi 600 milioni. Huo ni mshahara wa wiki moja wa mchezaji anayetoka nchi ya Afrika anayecheza Ulaya, Yaya Toure. Bajeti hii ya mshahara wa wiki wa Yaya Toure inainuaje soka?
Anayepaswa kutatua tatizo la foleni jiji la Dar es salaam akashindwa na kujiongezea posho za kijinga kila siku naye analaumu matokeo mabovu ya timu ya Taifa na viwango vibovu vya Simba, Yanga, Azam katika michuano ya Caf.
Kigogo wa TRA ni shabiki mzuri wa Arsenal. Anamsaidia yule Mfanyabiashara maarufu kukwepa kodi. Hajui kwamba pesa tunayopoteza ingesaidia uchumi wa nchi na michezo wa ujumla. Hapa huwa ananiacha hoi kweli kweli.
Lakini anauchekaje mchezo wa soka? Kama mchezo wa soka umefeli, kwani hajui ni kwa kiasi gani Tanzania imefeli katika kukusanya kodi nyingi miongoni mwa nchi za Afrika? Hapa si ndio nchi ambayo Mfanyabiashara anapewa miaka mitano ya kutolipa kodi mpaka ajue faida ya biashara yake? Wenyewe wanaita kwa kizungu Tax Holiday.
Kigogo wa Wizara nyeti ya ulinzi anamlinda Kigogo mwenzake aliyebaka mtoto wa kiume. Wakiimaliza kesi kituo cha Polisi wanaitana Serena Hoteli kupongezana kwa kula mishkaki huku wanacheki mechi ya Taifa Stars dhidi ya Ivory Coast TBC. Tukifungwa wanasema hatujui mpira na wachezaji wetu ni duni.
Unajiuliza, kwani mchezaji wa Tanzania si anatokana na mtoto wa Kitanzania? Mbona wametoka kumkandamiza mtoto wa Kitanzania? Naishia kucheka taratibu kwa uchungu.
Mchezaji mwenye kipaji kama Haruna Moshi ‘Boban’ hajaweza kung’ara Ulaya. Kuna tofauti gani na Mlima Kilimanjaro kushindwa kusaidia uchumi wa Taifa lake zaidi ya ilivyo sasa. Kuna tofauti gani na Mtanzania kufa njaa wakati ana ardhi kilomita nyingi zenye rutuba?
Mwisho wa yote tunaishi katika Taifa lililooza. Taifa lisilo na maadili katika uchumi, jamii na siasa. Kila unapowaza unakubali kwamba soka la Tanzania lipo chini na limeoza. Hatuonyeshi matumaini. Lakini niambieni ni wapi kuna matumaini na nidhamu?
Tatizo limebaki kwa Mtanzania mwenyewe. Hana uzalendo, ubunifu na umakini. Niambieni ni nani halaumiwi? Mwandishi wa habari? Mchezaji? Polisi? Rais? Mbunge? Mwanajeshi? Daktari? Mmachinga? Mfanyabiashara? Mkulima? Kila mtu haifanyi kazi yake sawa sawa.
Ni kweli. Tumekosa dira kama taifa. Hatujui tulipo wala tunapokwenda. Kabla haujamlaumu mwenzako jiulize, wewe unaifanyia nini nchi yako. je wewe Sekta yako ina maendeleo yanayostahili kabla ya kumnyooshea kidole mwingine?
Huwa nawaza sana. Daktari aliyemfanyia operesheni ya kichwa mtu anayestahili kufanyiwa operesheni ya goti, naye anamlaumu Polisi aliyechukua rushwa jana Kariakoo. Na yule polisi naye analaumu matokeo mabovu ya timu ya taifa. Na hata wachezaji wa timu ya taifa wanalalamika kuwa Rais anaendesha nchi hovyo. Rais naye ana malalamiko yake mengi kwa wananchi wa Mtwara kukataa gesi kutoka kusini.
kila mtu anamlaumu mwingine. Cheni ya lawama inakuwa ndefu, lakini mwisho wa siku ukweli unabakia pale pale kwamba Taifa limekosa maadili. Nani yuko salama na nani anafanya kazi yake kwa maadili makubwa?. Hakuna.
Kigogo anayeongoza Bandari anajifanya analaumu kwanini wachezaji wa Tanzania hawachezi Ulaya. Wala hajiulizi kwanini chini ya Bandari yake uchumi wa Tanzania usiongoze Afrika Mashariki na kati na baadhi ya nchi za Ulaya zisizo na Bandari.
Wabrazil wanakosea kwingine, lakini mpira wanajua. Wachina wanakosea katika mpira, lakini uchumi wanajua. Wamarekani wanakosea katika moja kidogo, lakini jingine wanafahamu. Ethiopia wana umaskini, lakini katika riadha wanapatia. Katika soka wanajitokeza.
Tanzania tunafahamu nini zaidi? Tumepatia wapi hadi tuseme mpira ni tatizo sana? wasomi na wananchi wa kawaida tuanze kuitafakari nchi kwa pamoja. Tusitafakari kwa mapande mapande. Tuna tatizo kila sehemu. Nani hajawahi kulaumiwa au kulaumu? Kila mtu tatizo nchi hii…

Share this:

 
Copyright © CHIWILEINC. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates