MASHIRIKA yasiyo ya kiserikali (NGOs) ambayo yatabainika yanaendelea kusambaza vilainishi kwa wanaume wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja, yatafutiwa usajili.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu aliyaandika hayo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa ‘facebook’.
Alisisitiza kuwa serikali italisimamia suala hilo kwa ukamilifu.
“Sijapiga marufuku matumizi ya vilainishi, ukweli nimepiga marufuku mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) kununua na kusambaza vilainishi kwa wanaume wanaojihusisha na mapenzi na wanaume wenzao na sababu nimeshazieleza,” aliandika na kuongeza:
“Na nafurahi kuwajulisha kuwa tayari baadhi ya mashirika hayo yameanza kutekeleza agizo hili kwa kuondoa vilainishi kwenye miradi yao. Nayapongeza sana. Niendelee kuyataka mashirika mengine kutii agizo hili ambalo tutalisimamia kwa ukamilifu.
“Serikali haitasita kuchukua hatua ikiwamo kuyafutia usajili mashirika yanayoendelea na miradi ya kusambaza vilainishi kwa wanaume wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja”.
Aliyataka mashirika hayo kushirikiana na serikali kupambana na maambukizi ya virusi vya Ukimwi kwa kujikita kwenye afya nyingine inayozingatia sheria za nchi na mila na desturi za Watanzania.
Akizungumza Dar es Salaam hivi karibuni, Waziri Ummy alisema uamuzi huo umechukuliwa baada ya kubaini matumizi ya vilainishi hivyo yanachochea kuongezeka vitendo vya ushoga ambavyo ni kinyume na sheria za nchi.
“Lengo pia ni kudhibiti maambukizi ya VVU kwa sababu katika wanaume wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja, asilimia 23 tayari wana maambukizi hayo.
“Tumebaini baadhi ya wadau wanaotekelezeka shughuli za makundi maalum wamekuwa wakikiuka taratibu za utendaji na kusambaza vilainishi hivyo.
Awali agizo hilo lilizua mjadala mkubwa katika mitandao ya jamii, wengi wakikosoa uamuzi huo wa Serikali kupiga marufuku vilainishi hivyo.
Walisema kwamba vinatumika katika mambo mengine mtambuka hususan hospitalini huku wengine wakisema viendo vya ushoga havichangiwi na kuwapo vilanishi bali ni mmomonyoko wa maadili uliotamalaki nchini
Post a Comment