Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alionya kwamba
wananchi wanalazimika kujenga utamaduni wa kuthamini kazi za wabunifu na
wasanii kwa kuona fahari kuzilipia bila ya shuruti pale wanapozitumia
jambo ambalo ni uungwana na kinyume chake inahesabika kuwa ni wizi.
Alisema
Serikali kupitia Ofisi ya Hakimiliki, Bodi ya Hakimiliki na Jumuiya ya
Hakimiliki Zanzibar { COSOZA } itaendelea kusimamia kazi za wabunifu na
wasanii ili kuona kuwa maslahi, nguvu na jasho lao halipotei bure
kutokana na ulaghai unaoendelea kufanywa na watu wanaozipora kazi zao.
Balozi
Seif Ali Iddi alitoa onyo hilo wakati wa hafla ya ugawaji wa Mirabaha
kwa Wabunifu na wasanii Zanzibar zilizofanyika katika Ukumbi wa Mikutano
wa Salama Bwawani Mjini Zanzibar.
Alisema
Serikali itaendelea kuchukuwa hatua za kisheria za kuwadhibiti wezi hao
wasiojali jasho la wenzao, lakini kazi hiyo inaweza kufanikiwa kwa
ufanisi zaidi endapo wabunifu na wasanii wenyewe watatoa ushirikiano
kwa taasisi zinazosimamia maslahi yao katika kudhibiti wizi wa kazi
zao.
“
Tushirikiane katika kuwasaka, kuwabaini na kuwaripoti katika vyombo
vinavyohusika wale wote watakaobainika wanatumia kazi zenu kinyume na
sheria na taratibu zilizowekwa “. Alisema Balozi Seif.
Alifahamisha
kwamba Serikali haipendi kuwabughudhi wananchi wake katika biashara
hata kidogo lakini hulazimika kuchukuwa hatua za kisheria mara moja
pale ambapo uvunjaji wa sheria unapobainika ili haki ipatikane kutokana
na sheria inavyochukuwa mkondo wake.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwazindua wabunifu na wasanii kuwa
wanapoingia kwenye mikataba pamoja na watumiaji wa kazi zao wahakikishe
kwamba makubaliano yao yanakuwa halali yanayozingatia misingi ya
hakimiliki katika biashara zao.
Balozi
Seif aliwataka wabunifu na wasanii wale na tahadhari wakati wa kuweka
saini Mikataba, wanakuwa na makubaliano na maelewano ya kweli ili
kuwepuka mizozo baina yao na wale wanaotiliana nao saini mikataba hiyo.
Balozi
Seif aliwasihi wamiliki wa vituo vya utangazaji kuheshimu haki na kazi
za wabunifu na wasanii wakielewa kwamba vituo vyao vinategemea kwa
kiasi kikubwa kazi hizo.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameishukuru na kuipongeza Ofisi ya Msajili
wa Hakimiliki kwa kusimamia vyema ukusanyaji na ugawaji wa Mirabaha na
kuitaka iendelee na utaratibu huo kwa kila mwaka.
Balozi
Seif aliiomba Ofisi hiyo kuandaa mpango maalum kwa wabunifu wa michoro
mbali mbali zikiwemo picha za ramani ili wafaidike moja kwa moja na
mirabaha kwa makusanyo badala ya utaratibu wa sasa wa makubaliano ya
mbunifu na mhitaji wa kazi husika.
Amewapongeza
wabunifu na wasanii wote wa Zanzibar waliopo na wale waliotangulia
mbele ya haki kwa kazi zao mbali mbali ambazo zimeitangaza na kuijengea
sifa Zanzibar katika medani ya Kimataifa.
Alisema
kazi za wabunifu na wasanii hao zimechangia kuelimisha, kuburudisha,
kuhamasisha na kuhifadhi utamaduni wa Taifa hili pamoja na kutoa ajira
kwa wananchi walio wengi hasa kundi kubwa la Vijana na hatimae kuchangia
uchumi wa Taifa.
“
Hatimiliki ukijumlisha na ubunifu na sanaa jawabu unalopata ni ajira
pamoja na ukuaji wa uchumi wa Taifa “. Alisema Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar.
Balozi
Seif alisema kutokana na umuhimu wa wabunifu na wasanii, Jumuiya ya
Kimataifa iliweka misingi mikuu na muhimu ya kufuatwa na nchi zote
wanachama katika kusimamia ulinzi, hadhi, haki na maslahi yao mkataba
ambao unasimamiwa na shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia
maslahi ya wabunifu na wasanii { World Intellectual Property
Organisation – WIPO }.
Alisema
Tanzania iliridhia mkataba huo wa Berne mwaka 1886 wakati Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar ikaridhia mkataba huo kwa kupitishwa sheria
nambari 14 ya mwaka 2003 yenye kusimamia masuala ya Hakimiliki.
“
Sheria hiyo ndio iliyounda Ofisi inayosimamia masuala ya Hakimiliki,
Bodi ya Hakimiliki na Jumuiya ya Hakimiliki maarufu COSOZA “. Alisema
Balozi Seif.
Akitoa
Taarifa Msimamizi na Afisa Mtendaji Mkuu wa Ofisi ya Hakimiliki
Zanzibar Bibi Mtumwa Khatibu Kheir alisema huo ni mgao wa pili wa
Mirabaha kwa wabunifu na wasanii wapatao elfu 1124 wa zanzibar.
Bibi
Mtumwa alisema Ofisi ya Hakimiliki imefanya kazi kubwa na nzuri kwa
kushirikiana na kamisheni ya Utalii pamoja na Mamlaka ya Uwekezaji
vitega uchumi Zanzibar { ZIPA } katika kuziunganisha kwa wateja kazi za
wabunifu na wasanii.
Hata
hivyo Msimamizi na Afisa Mtendaji Mkuu huyo wa Ofisi ya Hakimiliki
alitanabahisha kwamba wabunifu na wasanii wasiosajiliwa kamwe hawataweza
kufaidika na mgao wa Mirabaha inayotolewa.
Bibi
Mtumwa Khatibu Ameir aliwataja wabunifu na wasanii wanne waliokuwa
mfano mwaka huu kuwa ni pamoja na Bwana Khamis Juma, Bibi Mwapombe
Hiari, Bwana Mwalimu Ali Mwalimu na Marehemu Seif salim.
Mapema
akimkaribisha Mgeni rasmi Balozi Seif, Waziri wa Katiba na Sheria
Zanzibar Mh. Aboubakar Khamis Bakar alisema vipaji walivyokuwa navyo
wabunifu na wasanii wa
Zanzibar ni vyema vikaenziwa na kuheshimiwa kwa faida ya Taifa kwa jumla.
Waziri
Aboubakar alisema Zanzibar imepata umaarufu mkubwa Duniani kutokana na
ongezeko la vipaji vya wabunifu na wasanii wake wanaoonekana kuwa
kivutio kwa wageni na watalii mbali mbali wanafuatilia kazi za wabunifu
na wasanii hao.
Waziri
wa Katiba na Sheria Zanzibar aliwashukuru wachangiaji kutoka Taasisi
mbali mbali za Umma na zile binafsi wakiwemo pia watu maarufu kwa uamuzi
wao wa kusaidia kufanikisha kazi hiyo muhimu kwa taifa.
Post a Comment